Aug 29, 2023 06:55 UTC
  • Nchi 65 zashiriki kongamano la kuiunga mkono Palestina katika mji mtakatifu wa Karbala, Iraq

Mkutano wa kimataifa wenye anuani ya Wito wa Al-Aqsa umefanyika katika mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq, kwa kuhudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 65 duniani.

Mkutano wa Kimataifa wa Wito wa Al-Aqsa na kwa kaulimbiu ya "Palestina na Imam Hussein (AS)" ulifanyika kuanzia siku ya Jumapili hadi jana Jumatatu katika mji wa Karbala, Iraq kwa kuhudhuriwa na wanafikra na shakhsia wa kisiasa na kiutamaduni kutoka nchi 65 za dunia, kupitia kampeni ya Mpango wa Kimataifa wa Kurejea Palestina na chini ya usimamizi wa taasisi ya A'taba ya Hussein (AS).
Kwa mujibu wa televisheni ya Al-Mayadeen, katika mwendelezo wa mshikamano wa kimataifa kwa kadhia ya Palestina, kongamano maalumu lilifanyika mjini Karbala siku ya Jumapili kwa anuani ya "Wito wa Al-Aqsa" ambapo washiriki wake walisisitiza kuwa suala la Palestina ni medani kuu na ya kwanza ya vita kati ya watetezi wa uhuru duniani na madola ya kikoloni.

Karbala, Iraq yanakofanyika maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein AS

Kongamano hilo limetangaza upinzani wake kwa hatua ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kuwataka maulamaa wa Kiislamu na watetezi wa uhuru ulimwenguni kukabiliana na suala hilo.

Mwishoni mwa mkutano huu imesisitizwa kuwa, kuvivunjia heshima vitabu vitakatifu ikiwemo Qur'ani Tukufu kunatokana na uungaji mkono wa wazi wa pande zile zile zinazouunga mkono utawala wa Kizayuni.

Kongamano la kwanza la kimataifa la "Wito wa Al-Aqsa" chini ya kaulimbiu ya "Misingi ya harakati ya Imam Hussein na nafasi yake katika ukombozi wa Quds na mapinduzi ya taifa la Palestina" lilifanyika mwaka jana sambamba na kukaribia maombolezo ya Arubaini ya Imam Hussein AS huko Karbala, ambapo washiriki wa kongamano hilo walisisitiza juu ya kuendelezwa muqawama na mapambano huko Palestina na katika nchi nyingine za Kiislamu.../

 

Tags