Sep 25, 2023 13:12 UTC
  • OIC yatoa mwito wa kusitishwa jinai za utawala wa Kizayuni

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imelaani kushadidi jinai zinazofanywa na vikosi vya utawala ghasibu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina na kutaka kukomeshwa vitendo hivyo.

Taarifa iliyotolewa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani jinai ya karibuni kabisa ya Israel ya kuwauwa shahidi vijana wawili wa Kipalestina na vilevile kubomoa miundombinu ya kambi ya wakimbizi ya Nur al-Shams iliyoko mashariki mwa mji wa Tulkarm.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema bayana kwamba, hujuma na mashambulio ya utawala ghasibu wa Israel ni jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu pia imeitaka jamii ya kimataifa kuuwekea mashinikizo utawala ghasibu wa Israel ukiwa jeshi linaloukalia kwa mabavu ili kukomesha jinai na hujuma za mara kwa mara za utawala huo ghasibu wa Israel na jamii ya kimataifa kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.

 

Juzi pia Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ilitoa taarifa ya kulaani vikali vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

 Hivi karibuni, sambamba na maadhimisho ya sikukuu za Kiyahudi, mamia ya walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada wamekuwa wakiuvamia msikiti mtakatifu wa al-Aqsa na kufanya vitendo vya kichochezi.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.