Nov 01, 2023 03:02 UTC
  • Oman yataka Israel ibebeshwe dhima kwa jinai zake huko Gaza

Oman imeitaka jamii ya kimataifa iibebeshe dhima Israel kwa jinai zake za kutisha katika Ukanda wa Gaza, na pia dunia ichukue hatua za dharura za kukomesha mauaji ya halaiki ya Wapalestina wasio na hatia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Sayyid Badr bin Hamad Al-Busaidi alitoa mwito huo jana Jumanne katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kueleza kuwa, maafisa wa Israel wanapasa kufunguliwa mashitaka kwa kuwalenga raia katika Ukanda wa Gaza.

Amesema jamii ya kimataifa inapasa kuanzisha uchunguzi huru juu ya mauaji ya raia wa Palestina, na vile vile kwa utawala huo pandikizi kuzuia kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza ambao upo chini ya mzingiro.

"Mwishoye, ukweli utatawala, na dhulma itashindwa," ameongeza Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman katika ujumbe wake huo aliotuma kwenye mtandao wa X (Twitter). 

Badr amesisitiza kuwa, "Mauaji ya kimbari, adhabu ya jumla, kuwahujumu raia wasio na hatia, na kuzuia misaada ya kibinadamu kuifikia jamii inayostahiki ni jinai katika sheria za kimataifa."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Sayyid Badr bin Hamad Al-Busaidi

Mashambulizi ya kikatili ya kijeshi ya Israel dhidi ya Gaza, yaliyoanza tarehe 7 Oktoba kujibu operesheni ya kundi la muqawama la Palestina Hamas, yamesababisha vifo vya watu zaidi 8,500 wakiwemo watoto zaidi ya 3,500 wa Kipalestina.

Wakati huo huo, Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour ameonya juu ya kuendelea kuwa mbaya zaidi hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kueleza kuwa, "Gaza hivi sasa imegeuka jahanamu duniani."

Amesema mashambulizi ya kinyama ya Israel ni vita dhidi ya watoto wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza, na kuongeza kwamba katika kila dakika 5, mtoto mmoja anauawa shahidi katika eneo hilo lililozingirwa.

Tags