Dec 06, 2023 12:21 UTC
  • Hamas ina mpango kabambe wa kujihami katika vita na Israel

Afisa wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (muqawama) ya Palestina, Hamas, amesema harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Palestina yenye makao yake Gaza imeandaa mpango mkubwa wa kujihami katika kukabiliana na mashambulizi ya Israel, na kusisitiza kwamba umoja kati ya makundi ya muqawama wakati wa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa uliwashangaza makamanda wa kijeshi wa Israel.

Ali Baraka, mkuu wa Uhusiano wa Kitaifa wa Hamas Nje ya Nchi, ameiambia tovuti ya habari ya al-Ahed ya Lebanon kwamba: "Tuna uhakika kwamba tutaibuka washindi katika vita hivi. Tunawahakikishia wenzetu wa Palestina kwamba mapambano yana nguvu zinazohitajika kuwaachilia wafungwa wote wa Kipalestina."

Ameongeza kuwa jeshi la Israel limeshindwa kupata mafanikio yoyote katika vita vya nchi kavu dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Baraka amebainisha kuwa utawala ghasibu wa Israel ulianzisha mashambulizi ya nchi kavu huko Gaza baada ya idara zake za usalama kushtukizwa katika Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa. Amesema hadi sasa Israel haijaweza kufikia malengo yoyote iliyotangaza ambayo yalikuwa ni pamoja na kuangamiza Hamas, kuachiliwa wafungwa wake wote na kutimuliwa Wapalestina kutoka Gaza.

Kwingineko afisa wa ngazi ya juu wa Hamas amesema utawala haramu wa Israel "unazidi kuzama ndani na zaidi katika kinamasi cha Gaza", akisisitiza kuwa utawala huo ghasibu umeshindwa kupata ushindi hata mmoja baada ya siku 60 za vita katika eneo hilo linalozingirwa.

Osama Hamdan

Osama Hamdan, mwakilishi mkuu wa Hamas nchini Lebanon, aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu Beirut siku ya Jumanne, na kubainisha kuwa kundi la Hamas "limejiandaa vyema" kupigana bila kujali ni muda gani vita vya Israel vitaendelea.

Hamdan pia amewapongeza wapiganaji wa Brigedi ya al-Qassam, tawi la kijeshi la Hamas, ambao wanatetea haki za watu wa Palestina na ardhi yao, akisema "kila wakati wanamfanya adui kupata majeraha na hasara na kuifanya Gaza kuwa makaburi ya wavamizi.”