Jan 08, 2024 06:12 UTC
  • Amir wa Qatar: Mashambulio ya Israel Gaza yasimamishwe, usitishaji vita utekelezwe haraka

Amir wa Qatar amesisitiza juu ya kusimamishwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kutekelezwa haraka usitishaji vita katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Amir wa Qatar Sheikh Tamim Bin Hamad Al Thani ametoa sisitizo hilo katika mkutano aliofanya jana Jumapili na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken mjini Doha, na kuongeza kwamba kuna udharura pia wa kupelekwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo.
Sheikh Tamim amebainisha kuwa, kuna udharura mkubwa wa kupunguza mivutano ili kuhakikisha utulivu na usalama unapatikana katika eneo.
Jana hiyohiyo, na katika mazungumzo na Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan, Ayman al-Safadi, naye pia alisisitiza kusitishwa mara moja mashambulizi ya utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Gaza, kuwalinda raia, na kuhakiksha misaada ya kutosha na endelevu ya kibinadamu na ya matibabu inafikishwa kwenye maeneo yote ya ukanda huo.

Tangu ilipoanzishwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023, Marekani na nchi za Magharibi zinazoiunga mkono Ikulu ya White House zimekuwa zikiusaidia na kuuhami waziwazi utawala wa Kizayuni na kuzuia amani na utulivu kurejeshwa huko Gaza.

 
Marekani na Uingereza ni miongoni mwa nchi ambazo muda wote huu zimekuwa zikipiga kura ya kupinga maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kusimamisha vita katika Ukanda wa Gaza, na kinyume na madai ya uongo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pekee, ndiyo ambayo tangu ulipoanza uchokozi wa utawala haramu wa Israel, imetilia mkazo  ulazima wa kusitishwa vita, katika Ukanda wa Gaza.
 
Marekani, Uingereza na Ufaransa, zikiwa ni nchi zenye haki ya veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hazikuwa tayari kamwe kuchukua hatua ya kuwatetea watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kuzima moto wa vita na jinai za utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.../

 

Tags