Apr 21, 2024 02:17 UTC
  • Mauaji ya kimbari Ukanda wa Gaza na uwezekano wa  Qatar kuangalia upya sera zake za kigeni za usuluhishi

Muhammad bin Abdulrahman Al Thani Waziri Mkuu wa Qatar amesema kuwa nchi hiyo inatathmini upya nafasi yake kama msuluhishi kati ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas).

Qatar ni mojawapo ya nchi ndogo katika eneo la Asia Magharibi kwa sababu eneo lake ni zaidi ya kilomita 11,500 tu. Nchi hiyo ni ndogo lakini imekuwa ikitekeleza siasa za usuluhishi katika migogo mbalimbali ya eneo hili katika kalibu ya sera zake za nje. Sera hizo kwa upande mmoja zimedhihirisha taswira na sura chanya ya Qatar na kuiarifisha kama pande inayojaribu kurejesha amani; na kwa upande mwingine imeifanya Qatar kuwa na nafasi athirifu katika eneo linalokabiliwa na mizozo la Asia Magharibi. 

Nchi ya Qatar 

Usuluhishi wa Qatar hadi sasa umekuwa na matokeo chanya katika migogoro mbalimbali ya kikanda, ikiwa ni pamoja na Lebanon, Sudan, Palestina na Afghanistan.

Mbali na hilo, Qatar imekuwa msuluhishi kwa mara kadhaa kati ya Iran na Marekani na kubadilishana jumbe za kidiplomasia kati ya Tehran na Washngton. Kwa kuzingatia utendaji huo, kimsingi Qatar ni nchi ya kwanza ambayo mataifa makubwa duniani yanaitegemea katika kadhia na masuala mbalimbali ya eneo hili kwa ajili ya upatanishi na hata kwa ajili ya kuendesha mikutano mbalimbali ya kidiplomasia. 

Kuwa na uwezo wa kiuchumi pia kunaifanya Qatar kuwa nchi  iliyo na uwezo wa kuchukua nafasi na jukumu la usuluhishi. Pamoja na hayo, Waziri Mkuu wa Qatar hivi karibuni ameeleza kuwa nchi hiyo itaangalia upya nafasi yake ya upatanishi. Amebainisha haya  kuhusiana na vita vya Gaza. 

Mwezi wa saba wa mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza pia unaelekea kumalizika. Utawala huo hata hivyo hadi sasa haujafikia hata moja ya malengo yake makuu ya kijeshi katika vita hivyo yaani kuachiwa huru mateka wa upande wa utawala huo, si kwa njia ya kijeshi au njia za kidiplomasia. 

Qatar pamoja na Misri na Marekani zinafanya juhudi ili kufikiwa usitishaji vita kati ya Israel na Hamas na kuachiwa huru mateka wa Israel. Kushindwa kufikia lengo hilo kulipelekea hivi karibuni wawakilishi kadhaa wa Kongresi ya Marekani kutangaza kuwa Marekani inapasa kutazama upya uhusiano wake na Qatar kufuatia kufeli juhudi za upatanishi za Doha.  Wawakilishi wa Kongresi ya Marekani wamekosoa suala hilo ambapo kimsingi hatua ya Marekani ya kuunga mkono mauaji ya kimnbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza ni sababu kuu ya kugonga mwamba juhudi hizo za kisiasa kuhusu vita vya Gaza.

Israel inatekeleza mauaji ya kimbari Ukanda wa Gaza 

Inaonekana kuwa sababu inayowafanya wawakilishi wa Kongresi ya Marekani wawe na mtazamo mbaya kwa Qatar ni uhusiano kati ya Doha na haraktati ya Hamas. Qatar na  Hamas zina uhusiano wa karibu; na baadhi ya wawakilishi wa harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina pia wapo Qatar.  

Wanachotaka wabunge wa Kongresi ya Marekani ni kuwa Doha inapasa kutumia ushawishi wake kuilazimisha Hamas ikubali matakwa ya utawala wa Kizayuni na Marekani. Hili si suala ambalo viongozi wa Hamas watalikubali kwa sababu utawala wa Kizayuni unapaswa kukubali matakwa ya harakati hiyo ikiwa ni pamoja na kusitisha mauaji ya kimbari huko Ukanda Gaza. 

Kwa hiyo, Sheikh Muhammad bin Abdulrahman Al Thani amesema kuwa Doha imetumiwa vibaya na wale wanaojaribu kujipatia pointi za kisiasa. 

 

Tags