Apr 02, 2024 02:19 UTC
  • Sababu za utawala wa Kizayuni kulazimisha vita katika upande wa kaskazini

Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni, amesema kwamba utawala huo haramu utapanua operesheni zake za kijeshi katika eneo la kaskazini la ardhi zinazokaliwa kwa mabvu na kushambulia kila sehemu ya Beirut na Damascus ambapo Hizbullah ya Lebanon inaendeshea shughuli zake.

Matamshi hayo ya Waziri wa Vita wa utawala haramu wa Israel yana maana ya kutaka kueneza vita katika upande wa kaskazini na kutangaza vita dhidi ya Hizbullah ya Lebanon. Je, ni kwa nini Tel Aviv inafuatilia siasa hizo za kichokozi na je, zitatekelezwa kivitendo?

Sababu ya kwanza inatokana na hali inayotawala hivi sasa ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni anaona kwamba kuendelea kubakia kwake madarakani kunategemea kuendelea chokochoko na vita dhidi ya Wapalestina na mrengo wa muqawama katika eneo. Netanyahu kwa sasa anakabiliwa na mashinikizo makali kutoka kwa waandamanaji na wakosoaji wake ndani ya utawala huo, wanaomtaka aondoke madarakani mara moja.

Sababu nyingine ni kuhusiana na baraza la mawaziri lenye msimamo mkali la utawala huo. Baraza hilo lina watu wenye misimamo mikali  ya kufurutu ada ambao hawaamini hata kidogo njia za usuluhishi wa kidiplomasia na hivyo wanataka vita na migogoro eindelee. Watu hao wana ugomvi na mvutano mkubwa hata ndani ya baraza hilo lenyewe na wana hamu ya kuona kuwa mvutano huo unapanuliwa hadi kuwafikia maadui wao wa nje katika eneo.

Sababu nyingine inatokana na ufahamu usio sahihi wa Netanyahu kuhusu hali halisi ya eneo. Anadhani kwamba kwa kuiharibu Gaza, atakuwa ametoa pigo kubwa kwa Hamas.

Silaha za Hizbullah ya Lebanon

Netanyahu anafikiri kwamba kwa kuharibu Gaza na hasa mahandaki na njia za chini ya ardhi zinazoishia Misri, Hamas haitaweza kuwa tena tishio kwa Israel kwa miaka mingi. Kwa hiyo, kwa vile sasa ameingia katika vita hivi vikubwa na vya umwagaji damu katika eneo, anaweza pia kutoa pigo kali na kuidhoofisha pakubwa Hizbullah ya Lebanon. Pamoja na hayo, hata wakosoaji na wanafikra wengi ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu wanaamini kuwa dhana hiyo ya Netanyahu na mawaziri wake wenye misimamo mikali kuhusiana na suala hilo ni potofu kwa sababu nguvu ya kijeshi ya Hizbullah ya Lebanon haiwezi kulinganishwa na ya Hamas.

Kwa upande mwingine, tofauti na Gaza, ambayo ni ardhi iliyofungwa na kuzingirwa kila upande na adui Mzayuni, ngome ya Lebanon umeunganishwa na Syria na ardhi zake za magharibi. Kwa kutekeleza mashambulizi ya mabomu mfululizo nchini Syria, kama ilivyoshuhudiwa katika siku chache zilizopita, Israel inajaribu kuvuruga njia za Hizbullah kufikishiwa zana za kijeshi.

Sababu nyingine ni kwamba utawala wa Kizayuni unaamini kuwa kimsingi jumuiya ya kimataifa haina uwezo wa kuzuia vita na hujuma yake ya kichokozi dhidi ya pande nyingine katika eneo.

Kwa maneno mengine ni kuwa vita vya Gaza na mauaji ya kimbari ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Ukanda wa Gaza ambayo yanaendeshwa kwa uungaji mkono wa wazi wa nchi za Magharibi hususan Marekani, na Umoja wa Mataifa umeshindwa kabisa kuyasimamisha, utawala huo umemea pembe zaidi na kuanza kufikiria jinsi ya kueneza mgogoro na vita dhidi ya pande nyingine katika eneo. Vita vya Gaza ni alama ya kushindwa kukubwa kwa jumuiya ya kimataifa, na hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yake.

Licha ya matamshi ya Gallant na sababu zilizotajwa kuhusiana na suala hili, lakini inaonekana kwamba baraza la mawaziri la Netanyahu kwa sasa halina uwezo wa kupanua vita katika upande wa kaskazini wa ardhi unazozikalia kwa mabavu.

Tags