May 01, 2024 07:19 UTC
  • UN: Ukatili wa polisi ya Marekani dhidi ya watetezi wa Palestina unatia wasiwasi

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake juu ya unyanyasaji wa polisi wa Marekani dhidi ya wanafunzi wanaoiunga mkono Palestina.

Shirika la Habari la Iran (IRNA) limetoa ripoti na kusema  kuwa, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, alitoa taarifa jana Jumanne akieleza wasiwasi wake kuhusu ukatili wa askari usalama wa Marekani dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanaofanya maandamano nchini humo kuiunga mkono Palestina.

Akizungumzia kusimamishwa na kufukuzwa wanafunzi wanaoandamana wa vyuo vikuu vya Marekani, Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, ana wasiwasi kutokana na hatua zisizofaa za maafisa wa kutekeleza sheria katika vyuo vikuu vya Marekani.

Ripoti za vyombo vya habari vya Marekani  zinasema, polisi wa nchi hiyo wanawaburuza chini waandamanaji na kutumia gesi ya pilipili ili kuwatawanya wanafunzi wanaofanya maandamano ya amani ya kupinga mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza

Maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu ya kuunga mkono watu wa Palestina na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni waliyoanzia  katika Chuo Kikuu cha Columbia huko New York nchini Marekani, sasa yamepanuka na kuenea katika vyuo vikuu vingine vya nchi hiyo, kama Yale, New York, Harvard, Texas, na Southern California. Maandamano hayo yameenea katika vyuo vikuu vya nchi nyingine za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, Ujerumani, Canada, Uingereza na Australia.

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, Wapalestina 34,535 wameuawa shahidi na 77,704 wamejeruhiwa tangu tarehe 7 mwezi Oktoba  2023, wakati utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita dhidi ya wakazi wa Palestina wa Ukanda wa Gaza.

Tags