May 01, 2024 02:23 UTC
  • Kukaribia muda wa kutolewa hukumu ya mahakama mbili za kimataifa dhidi ya utawala wa Kizayuni

Sambamba na kuongezeka uwezekano wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kutoa hukumu ya kukamatwa maafisa kadhaa wa utawala wa Kizayuni kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita huko Gaza, gazeti la Times lilimeandika kuwa, kuna uwezekano pia kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC inajiandaa kutoa hati ya kukamatwa Netanyahu na maafisa wengine wa ngazi za juu wa Israel akiwemo Waziri wa Vita, Mkuu wa Majeshi na baadhi ya maafisa wa usalama wa utawala huo kwa kuhusika na vita hivyo.

Tofauti ya mahakama hizo mbili ni kuwa Mahakama ICC kimsingi hushughulikia kesi za watu binafsi kinyume na Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ambayo hushughulikia kesi za serikali.

Kwa sasa, Israel inakabiliwa na tuhuma za  mauaji ya halaiki katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki. Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zilizochukua misimamo mikali dhidi ya uvamizi wa utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza, na licha ya  kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni, ulifunga ubalozi wa utawala huo nchini humo hadi mashambulizi ya maghasibu hao huko Gaza yatakaposimamishwa.

Waziri Mkuu gaidi wa utawala wa Kizayuni

Mahakama ya Kimataifa ya Haki ina wajibu wa kuziainishia nchi majukumu yao ya kisheria kimataifa na kuainisha fidia zinazopaswa kutoa kwa uharibifu na hasara iliyosababishiwa upande mwingine. Bila shaka, Mahakama ya Kimataifa ya Haki haina mamlaka ya kuamua kuhusu uhalifu wa mtu binafsi kwa sababu suala hilo liko ndani ya mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama hiyo amekuwa akichunguza  jinai zote ambazo zinatekelezwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu tangu Juni 13,2014 hadi sasa.

Majina ya nchi 15 za Kiarabu yanaonekana katika orodha ya nchi zilizotia saini mkataba wa kimataifa wa kupinga jinai za mauaji ya umati, lakini kwa bahati mbaya baadhi ya nchi hizo  simezembea katika ufuatiliaji wa jinai za utawala wa Kizayuni, suala ambalo limeifanya Afrika Kusini kuanzisha mchakato wa mahakama dhidi ya utawala huo. Hata hivyo, inawezekana nchi kama vile Algeria, Misri, Iraq, Jordan, Kuwait, Lebanon, Saudi Arabia na Tunisia zikajiunga na Afrika Kusini katika kesi hiyo na hivyo kuanda uwanja wa nchi zinginezo zisizo za Kiarabu kuunga mkono kesi hiyo. Suala hilo bila shaka linaweza kupelekea kutolewa vifaa vyote muhimu vya kisheria na rasilimali kwa ajili ya kusaidia mchakato wa kesi hiyo.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya The Hague ndiyo mahakama pekee duniani ambayo ina uwezo wa kuwahukumu watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa kivita, mauaji ya halaiki na jinai dhidi ya binadamu. Mahakama hiyo haina jeshi la polisi, na badala yake, inategemea wanachama wake 124, ambao ni pamoja na nchi nyingi za Ulaya, kuwakamata watu waliohusika na jinai, kwa amri ya mahakama hiyo.

Israel si mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na haitambui mamlaka yake, lakini Palestina ilikubaliwa kuwa mwanachama wa mahakama hiyo mwaka 2015. Israel imewaua shahidi zaidi ya Wapalestina 34,000 na kuwajeruhi wengine zaidi ya elfu 77 katika mashambulizi yake ya kinyama ya takriban miezi saba huko Gaza.

Mashambulizi hayo pia yamepelekea zaidi ya watu milioni 2.3 kuwa wakimbizi, jambo ambalo limesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu katika eneo hilo. Ni kutokana na mauaji hayo ndio maana utawala wa Netanyahu umekuwa ukituhumiwa kutekeleza uhalifu wa kivita, jinai dhidi ya binadamu na mauaji ya halaiki huko Gaza. Tangu mwaka 2014 hadi sasa mahakama hiyo imefanya chunguzi za jinai 32 na chunguzi za awali zipatazo 500 kuhusiana na migogoro ya Gaza, na inatarajiwa kuwa maelfu ya tafiti nyingine zitafanyika kuhusiana na vita vya sasa, ambazo bila shaka zitakuwa ndefu na kubwa zaidi kuliko tafiti za sasa.

Baraza la Netanyahu

Moja ya mambo ambayo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai inaweza kumnasa Netanyahu kuhusika nayo na kuliweka baraza lake la mawaziri chini ya mashinikizo makubwa ya kimataifa ni suala la kuzuia misaada ya kibinadamu kuwafikia wakaazi wa Gaza.

Ni kwa sababu hiyo ndipo Karim Khan (Karim Asad Ahmed Khan), Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, akashambulia utendaji wa serikali ya Israel katika uwanja wa misaada ya kibinadamu na kusema kuwa Israel inapunguza kwa makusudi na kuvuruga mchakato wa kufikishwa misaada  muhimu huko Gaza, na kwamba hatua hii ni sawa na kutekeleza jinai za  kivita. Suala jingine ambalo Mahakama ya The Hague inaweza  kulitumia kuushinikiza utawala wa Kizayuni ni ukweli kwamba licha ya ombi la Mahakama ya The Hague, Israel haijawasilisha mbele ya mahakama hiyo nyaraka zozote zinazohitajika na za kutosha kuhusu vita na kushambuliwa maeneo nyeti na muhimu katika ukanda huo. Kutokana na hali hiyo, Mahakama ya The Hague, ikinukuu nyaraka za siri na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, imekubali kwamba Netanyahu anastahili kuwekwa kizuizini kwa kuzingatia uhalifu wa kivita aliofanya. Licha ya juhudi zisizo na kikomo za Israel na Marekani za kuzuia kutolewa kibali cha kukamatwa Netanyahu, wachambuzi wengi duniani wanatumai kuwa waranti hiyo itatolewa. Waranti hiyo haitamnasa Netanyahu tu, bali pia itawajumuisha Waziri wa Vita na Mkuu wa Majeshi, jambo ambalo iwapo litatimia bila shaka litasababisha tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijawahi kushuhudiwa tena kimataifa.