May 02, 2024 07:26 UTC

Polisi wa kutuliza ghasia wa Ufaransa jana walikabiliana kwa mabavu na washiriki wa maandamano katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) katika mji mkuu wa nchi hiyo, Paris.

Uongozi wa Polisi ya mji mkuu Paris umetangaza kuwa, watu 45 walitiwa mbaroni jana katika maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani. Polisi 15 wa kikosi cha kutuliza ghasia pia walijeruhiwa katika makabliano na waandamanaji. 

Polisi ya Paris imetangaza kuwa watu elfu 18 walishiriki katika maandamano hayo katika mji mkuu jana Jumatano huku chama cha wafanyakazi cha mrengo wa kushoto CGT kikiripoti kuwa watu 50,000 walishiriki katika maandamano hayo ya Labour Day.  

Polisi ya Ufaransa pia imetangaza kuwa, mwaka huu jumla ya watu 121,000 walishiriki katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi kote Ufaransa, huku chama cha wafanyakazi cha mrengo wa kushoto CGT kikatangaza kuwa watu 200,000 wameshiriki katika maadhimisho ya nchi nzima ya Siku ya Wafanyakazi Duniani. 

Waandamanaji huko Paris walikasirishwa zaidi na kupanda kwa gharama za maisha na ukosefu wa ajira. Baadhi ya waandamanaji walipeperusha bendera za Palestina kuonyesha mshikamano wao na watu wa Ukanda wa Gaza.

Mei Dei nchini Ufaransa na mshikamano na watu wa Gaza 

Katika maandamano ya jana ya Mei Mosi, polisi wa kutuliza ghasia nchini Ufaransa walitumia gesi ya kutoa machozi na virungu kuwatawanya waandamanaji kadhaa. 

Tags