Apr 22, 2024 06:18 UTC
  • Maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu yafanyika mjini Paris

Baada ya mabishano mengi na ruhusa iliyotolewa na mahakama ya kiidara ya Ufaransa, maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu yamefanyika huko Paris, mji mkuu wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la Kifaransa la Le Figaro maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu yalifanyika mjini Paris siku ya Jumapili, kuitikia wito wa jumuiya 51 kikiwemo chama cha France Unbowed.

Kabla ya hapo, Polisi ya Ufaransa ilikuwa imepiga marufuku kufanyika maandamano yoyote ya kupinga ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu.

Alhamisi iliyopita, Polisi ya Paris ilipiga marufuku maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu kwa kisingizio cha kile ilichokiita hatari kubwa ya kuvurugika utulivu katika jamii, lakini siku ya Ijumaa mahakama ya kiidara ya mji mkuu Paris ilibatilisha marufuku hiyo kutokana na kupingana vikali na kwa uwazi na uhuru wa watu binafsi.

Tangu vilipoanza vita vya kikatili na kinyama vya utawala haramu  wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza, wimbi la ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Uislamu limeongezeka ndani ya Ufaransa, na katika muda huo miji mbalimbali ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Paris imeshuhudia maandamano ya mara kwa mara ya wapinzani wa hali inayotawala nchini humo na waungaji mkono wa Palestina.

Tags