May 02, 2024 07:34 UTC
  • Kiongozi wa serikali ya mpito ya Chad atazamiwa kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa Jumatatu

Jenerali Mahamat Idriss Deby Itno, aliyetangazwa na jeshi miaka mitatu iliyopita kuwa kiongozi wa serikali ya mpito ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi wa Rais Jumatatu ijayo baada ya jeshi la nchi hiyo kuwakandamiza pakubwa wagombea wa upinzani.

Mpinzani mkuu wa Mahamat Derby katika uchaguzi wa Rais wa Jumatatu ijayo ni mwanasiasa kwa jina la Succes Masra kutoka chama cha mrengo wa kushoto cha Les Transformateurs.

Succes Masra

Katika mji mkuu wa Chad, N'Djamena mabango pekee yanayotazamwa ni yale yenye maandishi yanayosomeka MIDI, yaani kifupi cha Mahamat Deby.

Ni wagombea 10 tu kati ya 20 walioidhinishwa kugombea katika uchaguzi wa Rais wa Jumatatu ijayo huko Chad. Baraza la Katiba la nchi hiyo limewazuia wanasiasa mashuhuri kama vile waziri mkuu wa zamani, Albert Pahimi Padacké kugombea kiti cha urais katika uchaguzi ujao. 

Wakati huo huo vyama vichache vya  upinzani vilivyosalia vimetoa wito wa kususia uchaguzi ambao wameutaja kuwa una lengo la kuiingiza tena mamlakani familia ya Deby. 

Mwezi Februari mwaka huu, Yaya Dillo, kiongozi wa upinzani wa Chad aliyeonekana kuwa tishio kubwa katika uchaguzi mkabala wa Itno, aliuawa baada ya kuzuka mapigano katika makao makuu ya chama chake kati ya wafuasi wa chama hicho na maajenti wa usalama.

 

Tags