Apr 30, 2024 02:48 UTC
  • IRGC: Usaidizi wa nchi 10 duniani kwa Wazayuni haukufua dafu mbele ya Shambulio la Iran

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema nchi 10 ziliusaidia utawala wa Kizayuni katika ulinzi wa anga ili kukabiliana na operesheni ya Ahadi ya Kweli ya kuutia adabu utawala huo, lakini hatimaye Iran ya Kiislamu iliisambaratisha na kuishinda mifumo hiyo ya ulinzi ya nchi hizo zinazotajika.

Brigedia Jenerali Ramezan Sharif, ameyasema hayo katika maadhimisho ya Wiki ya Itikadi na Siasa ya IRGC na Jeshi la Kujitolea la Wananchi la Basij, alipozungumzia operesheni ya Ahadi ya Kweli ya kuutia adabuu utawala wa Kizayuni na akaongeza kuwa, operesheni hiyo ilitekelezwa kwa silaha zilizotengenezwa Iran na adhama yake ilikuwa kubwa kiasi kwamba maadui watalazimika kutumia muda mrefu kuchunguza namna ilivyotekelezwa.
 
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kuwa, operesheni ya Ahadi ya Kweli iliutia nguvu zaidi uungaji mkono kwa Palestina; na operesheni hiyo kali ilitekelezwa dhidi ya utawala ambao huko nyuma ulishajidai na kujigamba mara kadhaa kuwa ni ngome yenye usalama katika eneo.

Brigedia Jenerali Ramzan Sharif amekumbusha kuwa operesheni ya Ahadi ya Kweli haikuwa ya kushtukiza na akaongeza kuwa, iliporushwa ndege ya kwanza isiyo na rubani, adui Mzayuni na waungaji mkono wake walikuwa wakingojea kuendelea mashambulizi ya makombora ya Iran.

 
Msemaji huyo wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kueleza kuwa, mbali na wananchi Waislamu wa Iran, operesheni ya Ahadi ya Kweli iliwafurahisha pia Waislamu na watetezi wa uhuru kote duniani na akaongeza kuwa, nchini Iran Palestina ndiyo kadhia kuu ya Ulimwengu wa Kiislamu, na hivi sasa takribani miaka 80 imepita tangu kukaliwa kwa mabavu Palestina na utawala ghasibu wa Israel huku Marekani na waitifaki wake wakiwa wanaendelea kuuunga mkono utawala huo.
 
Jumatatu, Aprili 1, 2024, utawala wa Kizayuni ulifanya shambulio la kigaidi dhidi ya sehemu ya ubalozi wa Iran mjini Damascus lililopelekea kuuawa shahidi washauri saba waandamizi wa kijeshi wa Iran.
 
Kufuatia jinai hiyo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Iran alitamka kuwa hatua hiyo ya Tel Aviv ni sawa na kuishambulia ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kwamba, utawala wa Kizayuni lazima "utatiwa adabu".
 
Kufuatia agizo hilo, usiku wa kuamkia Jumapili ya tarehe 14 Aprili 2024, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilichukua hatua hiyo ya kuutia adabu utawala huo khabithi kupitia Operesheni ya Ahadi ya Kweli kwa kurusha ndege zisizo na rubani na makombora yaliyopiga vituo vyake muhimu vya kijeshi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina yaliyopachikwa jina bandia la Israel.../

 

Tags