May 01, 2024 06:54 UTC
  • Russia yalaani sera za kinafiki za Marekani kuhusu uchunguzi wa mahakama ya ICC dhidi ya Israel

Russia imekosoa vikali sera za kinafiki na kindumakuwili za Marekani kutokana na kupinga uchunguzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kuhusu uhalifu unaofanywa na Israel katika vita vyake vya miezi kadhaa dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza, na wakati huo huo inaunga mkono hati ya kukamatwa Rais Vladimir Putin iliyotolewa na mahakama hiyo hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova amesema katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram kuwa "Washington iliunga mkono kikamilifu, bali ilichochea utoaji wa vibali vya ICC dhidi ya uongozi wa Russia. Lakini, Marekani yenyewe haitambui uhalali wa mahakama hiyo ya ICC inapotaka kuchunguza uhalifu wake na vibaraka wake." Zakharova ameshutumu msimamo huo akiutaja kuwa "upuuzi wa kifikra."

Maria Zakharova

Mwezi Machi 2023, mahakama ya ICC yenye makao yake The Hague nchini Uholanzi ilitoa hati ya kukamatwa Rais wa Russia, Vladimir Putun, ikimtuhumu kuwa amefanya uhalifu wa kivita nchini Ukraine. Wakati huo, Rais wa Marekani, Joe Biden, alisema uamuzi wa ICC wa kutoa hati ya kukamatwa Putin ulikuwa wa haki.

Wakati huuo huo, wabunge wa Marekani wako katika harakati za kuandaa muswada dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iwapo itaamua kutoa hati za kukamatwa maafisa wa ngazi za juu wa Israel wanaotuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita huko Gaza.

Jumatatu iliyopita, katibu wa habari wa Ikulu ya White House, Karine Jean-Pierre alisema kuwa Washington haiungi mkono uchunguzi wa ICC kuhusu jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu zilizofanywa na Israel huko Gaza.

Mahakama ya ICC, ambayo inaweza kuwafungulia mashtaka watu binafsi kwa uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari, kwa sasa inafanya uchunguzi kuhusu uhalifu wa kivita unaoripotiwa kufanywa na jeshi la Israel dhidi ya raia wa Palestina wa Ukanda wa Gaza.

Zaidi ya Wapalestina elfu 34 wameuawa na makumi ya maelfu ya wengine wamejeruhiwa katika mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo huko Gaza.