Apr 30, 2024 11:00 UTC
  • Ghuba ya Uajemi ni nyumba yetu

Jumatatu ya jana tarehe 10 Ordibehesht, 1403 Hijria, sawa na Aprili 29, 2024 ilisadifiana na kumbukumbu ya kutimuliwa wakoloni wa Kireno katika maji ya kusini mwa Iran mwaka 1622 Miladia.

Siku hii inafahamika katika kalenda ya Kiirani kwa jina la jina la Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozii Muadhamu wa Mapinduzi ya Kislamu ameizungumzia Ghuba ya Uajemi na kusema kuwa, "Ghuba ya Uajemi ni Nyumba Yetu."

Ghuba ya Uajemi, ambayo ni njia kuu ya baharini, daima imekuwa na nafasi ya kipekee ya kisiasa na leo hii inajulikana kama njia kuu ya kimataifa ya majini ulimwenguni.

Katika miaka ya hivi karibuni, na kwa kuchochewa na ukoloni wa Magharibi, baadhi ya nchi za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi zimetaka kupotosha jina la Ghuba ya Uajemi; ilhali ukweli ni kwamba tokea tangu na tangu Ghuba ya Uajemi imekuwa ikijulikana kwa jina hilo.

Ukanda huo mpana wa majini uko kusini na kusini magharibi mwa Iran na karibu na mikoa ya Khuzestan, Bushehr na sehemu ya mkoa ya Hormozgan wa Iran, na una mpaka wa pamoja kwa urefu tofauti na nchi saba za Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, Iraq, Saudi Arabia, Oman, Qatar na Kuwait.

Ingawa wavamizi waliondoka Ghuba ya Uajemi, lakini siku zote wamekuwa wakitokwa na mate ya uchu na tamaa kwa eneo hili la kimkakati. Uchu na tamaa yao inatokana zaidi na rasilimali kubwa ya nishati inayopatikana katika eneo hili.

 

Pamoja na kuwa, madola ya kigeni yanaeleza sababu ya kuwepo kwao kijeshi katika nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi kuwa ni kudhamini usalama wa eneo, lakini ukweli wa mambo ni kuwa, uwepo wao katu haujawa na matokeo yanayopigiwa upatu.

Hali ya Iraq katika kipindi cha miaka 24 iliyopita ndiyo ushahidi wa wazi zaidi katika uwanja huu kwamba, uwepo wa madola ya kigeni hususan Marekani haujapelekea kupatikana usalama wa eneo na wa nchi za Ghuba ya Uajemi.

Uungaji mkono wa pande zote unaotolewa na Marekani kwa utawala ghasibu wa Israel unaoukalia kwa mabavu Quds katika mauaji ya halaiki ya hivi sasa huko Gaza pia ni thibitisho kwamba, kuwepo Marekani katika Ghuba ya Uajemi sio sababu ya usalama, bali ni sababu kuu ya kuenea ukosefu wa usalama katika eneo hili.

Akizungumza kwa mnasaba wa Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi, Admirali Alireza Tangsiri Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema, mkakati wa Iran ni kuendeleza amani, usalama na udugu katika Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz. Akiashiria umuhimu wa kistratijia wa eneo hilo la bahari, Tangsiri amesema, maji ya kina kirefu zaidi kwenye pwani ya Ghuba ya Uajemi na njia bora za maji ziko upande wa Iran. Ameongeza kuwa Ghuba ya Uajemi ina nafasi muhimu kiuchumi, kwani asilimia 40 ya gesi ya dunia na asilimia 62 ya mafuta vinapatikana katika eneo hili. Kadhalika amesema, kanda hiyo ni "muhimu sana" linapokuja suala la usalama, akisisitiza kwamba, Iran inasisitiza kuwasilisha ujumbe wake wa amani na urafiki kwa nchi zote za kikanda. Iran inataka kuweka usalama kamili katika Lango Bahari la Hormuz na imezihakikishia usalama meli 83 zinazopita kwenye mkondo huu wa maji kila siku.

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, hakuna hata kesi ndogo ya ukosefu wa usalama katika mipaka ya pwani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi jirani. Nguvu ya kijeshi na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia vinatumika kwa ajili ya usalama wa Ghuba ya Uajemi, kama ambavyo sambamba na uvamizi wa Iraq na magaidi wa ISIS, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa nchi ya kwanza kujitokeza na kusaidia nchi hiyo jirani katika Ghuba ya Uajemi.

Ni kwa muktadha huo, ndio maana, Admirali Alireza Tangsiri Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesisitiza kuwa: "Tulitoa ujumbe wa amani, urafiki na udugu kwa nchi za Kiislamu za eneo na kusisitiza manufaa ya pande zote na nchi za eneo hili. "