Apr 01, 2024 10:44 UTC
  • Jeremy Corbyn
    Jeremy Corbyn

Kiongozi wa zamani wa chama cha Labour nchini Uingereza amezikosoa nchi za Magharibi - hasa Marekani na Uingereza - zinazoendelea kuipatia Israel silaha za kuwaua Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, na kusema kuwa nchi hizo zinakiuka sheria za kimataifa.

Jeremy Corbyn, ambaye kwa sasa ni mwakilishi katika Bunge la Uingereza amesisitiza kuwa, kuendelea serikali ya Uingereza kuiuzia Israel silaha kunaifanya mshirika katika jinai na uhalifu unaofanywa dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Corbyn amesema kuwa baadhi ya wajumbe wa Bunge la Uingereza wameitaka Wizara ya Mambo ya Nje kuweka wazi na kuchapisha ushauri wa kisheria unaothibitisha kuwa Israel inakiuka sheria za kimataifa katika vita vyake dhidi ya watu wa Gaza.

Awali, gazeti la The Observer, likimnukuu Alicia Cairns, mkuu wa Kamati ya Masuala ya Kigeni katika Bunge la Uingereza la House of Commons, lilifichua kwamba serikali ya nchi hiiyo haikuchapisha ushauri wa kisheria iliopewa, na inaendelea kuipatia silaha Israel.

Kwa kuzingatia hayo, Jeremy Corbyn anasema, serikali ya Uingereza imekiuka sheria za kimataifa kwa kuuza silaha kwa Israel, na pia kwa kubadilishana habari za kijasusi na Israel.

Maelfu ya Wapalestina wa Gaza wameuawa na jeshi la Israel kwa silaha za Marekani, Uingereza na Ujerumani

Kiongozi huyo wa zamani wa chama cha Labour amekumbusha mienendo ya waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair, ambaye alisema kuwa alijulishwa kwamba kushiriki London katika uvamizi dhidi ya Iraq hakukuwa halali, lakini alipuuza suala hilo, na kusema: Kinachofanywa sasa na serikali katika vita vya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza ni marudio ya kile kilichotokea katika uvamizi wa Iraq. Jeremy Corbyn ameongeza kuwa ukiukwaji wa sheria katika kesi ya Gaza uko wazi zaidi.

Kwa upande mwingine, Corbyn amesema kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Cameron, na Rais wa Marekani Joe Biden wanalia machozi ya mamba kwa watu wa Gaza, lakini wanaendeleza uhusiano wao wa karibu na Israel na Waziri Mkuu wake, Benjamin Netanyahu.

Tags