Apr 30, 2024 02:47 UTC
  • Balozi zote za Israel zawekwa kwenye hali ya tahadhari kuhofia waranti wa ICC wa jinai za vita vya Ghaza

Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa Kizayuni wa Israel imeziagiza balozi zake duniani kote kuwa tayari kwa madhara yanayoweza kutokea iwapo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) itatoa waranti wa kukamatwa maafisa wa utawala huo kwa uhalifu wa kivita na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Wizara hiyo imeeleza katika taarifa kwamba kuna "uvumi" unaoenea kuhusu uwezekano wa kutolewa na ICC hati za kukamatwa vigogo wa kisiasa na kijeshi wa Israel.
 
Kutokana na kuwepo uvumi huo, taarifa hiyo imesema, waziri wa mambo ya nje wa Israel Israel Katz ameripotiwa kuzielekeza balozi zote za utawala huo wa Kizayuni duniani kujiandaa mara moja na matukio yanayohusiana na alichokiita chuki dhidi ya Wayahudi na Israel.
 
Katz ameyaagiza pia mashirika ya Kiyahudi nje ya nchi kuchukua hatua hizo za tahadhari za kukabiliana na matukio hayo.
 
Waziri huyo wa utawala wa Kizayuni amenukuliwa akisema Israel "inatarajia mahakama kujizuia" kutoa vibali vya kukamatwa viongozi wake.

Utawala ghasibu wa Kizayuni una hofu kubwa ya kutolewa na Mahakama ya ICC hati za kukamatwa viongozi wake wakuu wa kijeshi na wa serikali, hasahasa waziri wake mkuu Benjamin Netanyahu, kwa kuhusika na jinai za kivita katika mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na jeshi la utawala huo huko Ukanda wa Ghaza.

 
Zaidi ya Wapalestina 34,400 wameshauawa shahidi tangu Oktoba 7 hadi sasa huko Ghaza wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na wengine 77,575 wamejeruhiwa, mbali na uharibifu mkubwa uliofanywa jeshi la Kizayuni kwa miundombinu na majengo ya kiraia sambamba na kuwadhikisha kwa njaa Wapalestina wa eneo hilo.
 
Utawala wa Kizayuni umefunguliwa mashtaka ya kuhusika na mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ. Uamuzi wa muda uliotolewa na mahakama hiyo mwezi Januari uliiamuru Tel Aviv isitishe vitendo vya mauaji ya kimbari na kuchukua hatua za kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia raia huko Ghaza, lakini hadi sasa utawala huo umekaidi kutekeleza maagizo hayo.../

 

Tags