Feb 19, 2024 11:08 UTC
  • Israel kuruhusu Wapalestina waliopindukia miaka 70 tu kuingia Msikiti wa Al Aqsa wakati wa Ramadhani

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeidhinisha mpango wa kuwawekea vizuizi vikali Wapalestina wanaoishi kwenye ardhi zilizoanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948 na wa mji wa Baitul Muqaddas (Jeruselem) vya kuingia kwenye Msikiti wa Al Aqsa wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, utakaoanza wiki ya pili ya mwezi ujao wa Machi.

Waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu alitoa idhini yake jana Jumapili kwa mapendekezo ya waziri wa usalama wa taifa mwenye misimamo ya kupindukia ya chuki Itamar Ben-Gvir, licha ya shirika la usalama wa ndani la utawala huo kuonya kwamba kuwawekea vizuizi Wapalestina wasiingie katika Msikiti wa Al Aqsa wakati wa Ramadhani kutakuwa sawa na kumimina petroli kwenye moto. 

Ben-Gvir ametaka baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni liwaruhusu Wapalestina wenye umri wa zaidi ya miaka 70 tu wanaoishi Baitul Muqaddas na maeneo yaliyoanza kukaliwa kwa mabavu mwaka a1948 kuingia kwenye Msikiti wa Al-Aqsa katika mwezi huo mtukufu.

Itamar Ben-Gvir

Chaneli ya 13 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imetangaza kuwa, "licha ya onyo lililotolewa na Shin Bet (shirika la usalama wa ndani) juu ya machafuko yanayoweza kutokea kati ya Wapalestina wa ndani ya Israel na polisi wa Israel, Netanyahu amekubali pendekezo la waziri wa usalama wa taifa Itamar Ben-Gvir la kuwawekea vizuizi vikali zaidi waumini wa Palestina watakaotaka kwenda kufanya ibada katika Msikiti wa Al Aqsa katika mwezi ujao wa Ramadhani".

Kwa mujibu wa chaneli hiyo, serikali ya Netanyahu itatoa uamuzi rasmi juu ya suala hilo mnamo siku chache zijazo.

Ikivinukuu vyanzo ambavyo haikuvitaja, chaneli ya 13 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imesema: "kuingia waumini wa Kipalestina kwenye Msikiti wa Al Aqsa wakati wa Ramadhani kutakuwa na kikomo".

Katika kipindi cha siku mbili zilizopita, vyombo kadhaa vya habari vya utawala haramu wa Israel, ikiwa ni pamoja na Chaneli12 vimeripoti kuwa Shin Bet imeuonya utawala huo kwamba kuwazuia Wapalestina wasiingie katika Msikiti wa Al Aqsa wakati wa Ramadhani "kunaweza kusababisha machafuko makubwa."

Shirika hilo la usalama wa ndani la Israel limetahadharisha kuwa uamuzi huo unaweza kusababisha machafuko "hatari" zaidi kuliko yale yaliyotokea Baitul Muqaddas, Ukingo wa Magharibi, na maeneo ya kandokando yake mnamo mwaka 1948 wakati ilipotangazwa kuasisiwa kwa utawala huo wa Kizayuni.../

 

 

 

 

Tags