May 06, 2024 12:09 UTC
  • Ujumbe wa Umoja wa Ulaya wasema 'mifumo yenye nguvu zaidi' imeshindwa kukabiliana na Wayemen

Kamanda wa operesheni za kikosi cha wanamaji cha Umoja wa Ulaya amekiri kuhusu uwezo mkubwa wa kijeshi wa Yemen katika eneo la Bahari Nyekundu.

Katika mkutano wa siri na wawakilishi wa kidiplomasia wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels wiki iliyopita, Kamanda Vasileios Gryparis, raia wa Ugiriki ameelezea wasiwasi wake juu ya uwezo wa vikosi vya Yemen ambavyo vimekuwa vikiendesha operesheni za kulipiza kisasi dhidi ya Israeli kwa ajili ya kuunga mkono watu wa Palestina. Kamanda huyo amesema vikosi vya Yemen vilifanikiwa kwa mara ya kwanza "kushinda ulinzi wa anga wa Umoja wa Ulaya na kuharibu meli ya kubeba mizigo ya biashara, kwa kutumia kundi la ndege zisizo na rubani" mnamo Aprili 29.

Katika kuonyesha mshikamano na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa, wanajeshi wa Yemen wamelenga meli zenye wamiliki wanaohusishwa na Israel au zile zinazokwenda na kutoka katika bandari zilizoko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu(Israel), zinazopitia katika Bahari Nyekundu.

Jeshi la Yemen likijaribu kusimamisha meli inayoelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu

Mwezi Disemba mwaka jana, Marekani iliunda muungano wa kuzuia mashambulizi ya Yemen dhidi ya Israel.

Mbali na muungano huo unaoongozwa na Marekani, Umoja wa Ulaya nao una kikosi kinacholenga kulinda meli za Wamagharibi katika Bahari Nyekundu.

Marekani na Uingereza pia zimekuwa zikifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Yemen kama njia ya kujaribu kuishinikiza nchi hiyo isitishe mfululizo wa operesheni ambazo imekuwa ikizitekeleza  kwa ajili ya kuwaunga mkono watu wa Gaza.

Yemen imekuwa ikifanya operesheni dhidi ya meli za kivita za Uingereza na Marekani ambazo zimetumwa kwenye Bahari Nyekundu kukabiliana na mashambulizi ya Yemen.

Gryparis amesema EU inatumia mifumo ya kisasa ya ulinzi, lakini pamoja na hayo mifumo hiyo yenye nguvu kubwa inasalimu amri mbele ya kundi kubwa la ndege zisizo na rubani.

Israel inaendesha vita vya mauaji ya halaiki huko Gaza tangu Oktoba 7 baada ya kundi la muqawama la Hamas kutekeleza Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya utawala huo wa kibaguzi ikiwa ni katika kulipiza kisasi kwa ukatili wake wa kupindukia dhidi ya watu wa Palestina.