May 23, 2021 11:24 UTC
  • Baada ya kushindwa katika vita vya Gaza Wazayuni wavamia Msikiti wa al Aqsa, wawazuia Wapalestina kufanya ibada

Hali ya wasiwai imetanda tena katika viwanja vya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina kutokana na hujuma ya walowezi wa Kizayuni wanaowashambulia raia wa Palestina wanaoelekea eneo hilo kwa ajili ya ibada baada ya jeshi la utawala katili wa Israel kushindwa kufikia malengo yake katika vita vya siku 12 huko Gaza.

Ripoti zinasema kuwa, zaidi ya walowezi 125 wamevamia viwanja vya Msikiti wa al Aqsa mapema leo Jumapili wakipewa himaya na ulinzi na jeshi la Israel na wamewapiga na kuwaudhi Waislamu wa Kipalestina waliokuwa wakielekea eneo hilo kwa ajili ya ibada.

Vilevile wanajeshi wa Israel wamewatia nguvuni wahudumu 5 wa Msikiti wa al Aqsa na vijana watatu wa Kipalestina na kuwaachia wawili miongoni mwao baadaye.

Machafuko mapya katika viwanja vya Msikiti wa al Aqsa yameanza baada ya wanajeshi wa Israel kumkamata na kumpiga kijana moja wa Kipalestina aliyekuwa kati ya raia waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala na kuwapiga wenzake waliojaribu kumtetea.

Mapema leo pia jeshi la Israel liliweka vizuri vya barabarani na kuwazuia Wapalestina kuelekea kwenye Msikiti wa al Aqsa kwa ajili ya ibada. Makumi ya Wapalestina pia wametiwa nguvuni katika machafuko hayo.

Al Aqsa

Kufuatia hali hiyo Ofisi ya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati na kutahadharisha kuwa yanayojiri katika Msikiti wa al Aqsa yumkini yakaibua tena vita baina ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Taarifa ya ofisi ya Rais wa Palestina imelaani uvamizi unaoendelea kufanywa na askari wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa na kitongoji cha Sheikh Jarrah katika mji wa Quds na kuitaka jamii ya kimataifa iingilie kati.

Imesema hujuma ya Wzayuni dhidi ya msikiti huo mtakatifu ni dharau kwa matakwa ya jamii ya kimataifa na kebehi kwa hisia za Waislamu zaidi ya milioni moja na nusu.

Tags