Aug 29, 2021 03:48 UTC
  • Mkutano wa Baghdad, kiwango cha ushiriki na malengo yake

Mkutano wa nchi jirani na Iraq umeanza leo Jumamosi tarehe 28 Agosti mjini Baghdad.

Iran, Saudi Arabia, Uturuki, Kuwait, Imarati, Jordan, Misri na Qatar zimealikwa katika mkutano huo. Iraq pia imezialika nchi 5 wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushiriki katika mkutano huo na taarifa zinasema kuwa, nchi hizo zitawakilishwa na mabalozi wao. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameamua kushiriki yeye mwenyewe katika mkutano huo wa Baghdad.

Moja kati ya maudhui muhimu za mkutano huo ni kiwango cha ushiriki wa nchi zilizoalikwa. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inawakilishiwa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Hossein Amir-Abdollahian. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh amesema, Waziri Hossein Amir-Abdollahian anaongoza ujumbe wa Iran katika mkutano wa Baghdad. Inasemekana kuwa Saudi Arabia na Uturuki pia zinawakilishwa na mawaziri wa mambo ya nchi za nje katika mkutano huo. Nchi za Jordan, Misri na Qatar zinawakilishwa na viongozi wa nchi hizo, na Kuwait imetangaza kuwa, Waziri Mkuu wa nchi hiyo ndiye atakayeiwakilisha katika mkutano wa Baghdad. Bado haijajulikana Imarati inawakilishwa na kiongozi wa ngazi gani katika mkutano huo. 

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian

Maudhui nyingine muhimu kuhusu mkutano wa Baghdad ni kutoalikwa Syria. Hii ni licha ya kwamba, Syria inashirikiana mpaka ya nchi mwenyeji, yaani Iraq. Kuhusiana na suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Fuad Hussein anasema: "Suala la Syria ni tata na lenye kuzusha hitilafu na haliko mikononi mwa serikali ya Baghdad. Iraq ina uhusiano mzuri na Syria, na uhusiano wa pande mbili hizi haujawahi kuwa mzuri sana kuliko ulivyo hivi sasa." 

Lengo la serikali ya Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al Kadhim la kuitisha mkutano wa sasa mjini Baghdad pia ni miongoni mwa madhui muhimu zinazomulikwa na duru za kisiasa na vyombo vya habari. Japokuwa baadhi ya wachambuzi wanasema ajenda kuu ya mkutano huo ni kujadili masuala muhimu ya kikanda, lakini inaonekana kuwa, masuala ya kiuchumi yanapewa kipaumbele zaidi.

Al Kadhimi ambaye amekuwa Waziri Mkuu wa Iraq tangu mwezi Mei mwaka jana amejikita zaidi katika suala la mahusiano ya kigeni. Hadi sasa serikali ya Iraq imefanya vikao vya pande tatu na maafisa wa serikali za Misri na Jordan. Mbali na hayo mwezi Aprili mwaka huu Waziri Mkuu huyo wa Iraq alifanya safari katika nchi mbili tajiri za Kiarabu yaani Saudi Arabia na Imarati kwa lengo la kuzihamasisha kuwekeza nchini Iraq.

Mkutano wa Baghdad

Katika mkutano wa sasa wa Baghdad pia al Kadhimi anafanya jitihada za kuzihamasisha nchi washiriki kwa ajili ya kuwekeza nchini Iraq na kusaidia uchumi wa nchi hiyo. Mkuu wa kamati ya maandalizi ya mkutano wa Baghdad, Nizar al Hamdullah anasema: "Mktano huu unafuatilia zaidi malengo ya kiuchumi na haujadili kabisa hitilafu zilizopo baina ya nchi washiriki." Ameongeza kuwa nchi zilizoalikwa zina uzoefu mzuri katika nyanja za uchumi, viwanda na uwekezaji, na kwamba Iraq inataka kuvutia wawekezaji hususan katika sekta ya kilimo na viwanda.

Mkutano wa sasa wa Baghdad unafanyika siku 45 kabla ya uchaguzi wa mapema wa Bunge uliopangwa kufanyika tarehe 10 Oktoba. Inaonekana kuwa, al Kadhimi pia anatumia mkutano huo kama turufu ya kisiasa kwa ajili ya uchagzi huo.      

Tags