Oct 24, 2022 07:31 UTC
  • Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan asisitiza kupatiwa ufumbuzi kadhia ya Palestina

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan amesisitiza kuwa, kupatiwa ufumbuzi kadhia ya palestina ni ufunguo wa kutatuliwa matizo ya eneo la Asia Magharibi.

Ayman Safadi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan sambamba na kusisitizia udharura wa kupatiwa ufumbuzi kadhia ya Palestina ametoa mwito wa kukomeshwa uvamizi, hujuma na mashambulio ya wanajeshi wa utawala ghasibu wa Istrael dhidi ya miji na vijiji vya Wapalestina.

Waziri Safadi ambaye nchi yake ya Jordan imekuwa mstari wa mbele kutangaza himaya na uungaji mkono wake kwa Wapalestina ametahadharisha juu ya kutokuweko muelekeo wa kisiasa kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi wa kuwekko mataifa mawili katika mzozo wa Palestina na Wazayuni maghasibu.

 

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jordan alinukkuliwa pia hivi karibuni akisema kuwa, hakuna matumaini yoyote ya kumalizika vita na kupatikana amani, maadamu utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Tags