Dec 07, 2022 03:13 UTC
  • Al Jazeera yawasilisha mashtaka ya mauaji Shireen kwenye mahakama ya kimataifa ya ICC

Mtandao wa Habari wa Al -Jazeera umetangaza kuwa umewasilisha kesi ya mauaji ya mfanyakazi wake, Shireen Abu Akleh, katika Mahakama ya Jinai ya Kimataifa huko Hague.

Hatua hiyo imechukuliwa miezi 6 tangu Shireen Abu Akleh alipouawa kinyama kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Israel baada ya timu ya masuala ya sheria ya mtandao wa al Jazeera kufanya uchunguzi sahihi na wa kina katika kesi hiyo, na kufichua ushahidi mpya uliotegemea maelezo ya mashuhuda na uchunguzi wa idadi kubwa ya video na ushahidi wa jinai unaohusiana na kesi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na al Jazeera imethibitisha kwamba, ushahidi mpya uliotokana taarifa za mashahidi na kanda za video unaonyesha wazi kuwa Shireen Abu Akleh na wenzake walilengwa kwa risasi za moja kwa moja na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel, na kwamba madai ya viongozi wa Israeli kwamba aliuawa wakati wa mashambulizi baina ya pande mbili hayana msingi wowote.

Mtandao wa al Jazeera umesema kuwa, ushahidi uliowasilishwa ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa mahakama ya ICC unathibitisha kwamba hakukuwa na mapigano au ufyatuaji wa risasi katika eneo ambako Shireen alikuwa, isipokuwa risasi ambazo zilimlenga yeye na wenzake moja kwa moja kutoka kwa askari wa Israel. 

Al Jazeera imekaribisha hatua ya jamii ya kimataifa, mashirika ya kutetea haki za binadamu na taasisi za kutetea uhuru wa vyombo vya habari ya kufuatilia ipasavyo kesi hiyo na kuendelea kutoa wito wa kuwajibishwa wale wote waliohusika na uhalifu huo mbaya.

Mwezi Mei mwaka huu mwandishi wa habari ya televisheni ya al Jazeera ya Qatar, Shireen Abu Akleh, 51, alipigwa risasi kichwani na kuuliwa kikatili na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakati akiwa kwenye kazi yake ya kuripoti uvamizi wa kijeshi wa jeshi la Israel katika kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Jenin.

Mwezi Junu mwaka huu pia Umoja wa Mataifa umesema taarifa ulizokusanya zinaonesha kuwa, Shireen Abu Akleh, mwandishi wa habari wa televisheni ya al-Jazeera ya Qatar aliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Israel.

Shireen Abu Akleh baada ya kupigwa risasi na askari wa Israel

Vilevile uchunguzi mpya wa gazeti la Marekani la New York Times umethibitisha kuwa risasi iliyomuua mwandishi wa habari wa televisheni ya Al Jazeera ya Qatar, Shireen Abu Akleh, ilifyatuliwa na mwanajeshi wa kikosi maalumu cha Israel, katika eneo ambalo halikuwa na mwanamgambo hata mmoja wa Kipalestina.

Gazeti hilo la Marekani limedokeza kuwa risasi iliyomuua Shireen ilifyatuliwa kutoka eneo walipokuwa wanajeshi wa Israel.

Tags