Apr 11, 2023 03:03 UTC
  • Spika wa Bunge la Iran: Uchokozi wa utawala wa Israel unathibitisha utambulisho wake wa kifashisti na kibaguzi

Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu, Bunge la Iran, amesema vitendo vya kichokozi vilivyofanywa hivi karibuni na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu vinadhihirisha tabia ya utawala huo wa kifashisti na ubaguzi wa rangi.

Mohammad Baqer Qalibaf aliyasema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa mtandaoni wa Kamati ya Palestina ya Umoja wa Mabunge ya Nchi Wanachama wa OIC (PUIC) Jumatatu, ambao ulihudhuriwa na maspika kadhaa wa bunge kutoka nchi mbalimbali za Kiislamu.

Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa: "Hatua zinazochukuliwa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa la Palestina ni pamoja na  jinai zake ... hasa katika miji ya Jenin na Nablus. Halikadhalika  pia utawala wa Israel unatekeleza juhudi za kuwakandamiza Wapalestina katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na kubadilisha demografia yake sambamba na kutekeleza sera  ubaguzi wa rangi.”

Qalibaf amebainisha kuwa wakati utawala wa Kizayuni ukikabiliana na matatizo yake ya ndani, "unajaribu kuficha udhaifu na tofauti za ndani ya utawala huo kwa kuendeleza jinai dhidi ya Wapalestina, [yakiwemo] mauaji, mauaji ya halaiki, kuvamia maeneo matakatifu na kuyachoma moto."

Kwa mara nyingine tena, Qalibaf amesisitiza kuhusu sera imara za Iran za kuunga mkono kadhia ya Palestina na kuongeza kuwa, mabunge ya nchi za Kiislamu lazima yachukue nafasi katika kuweka mwelekeo wa sera za serikali za Kiislamu kuhusiana na Palestina.

Spika wa Bunge la Iran ameongeza kuwa, "Viongozi watenda jinai wa utawala wa Kizayuni wanajaribu kuwazuia vijana wa Palestina kuzirejesha ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na kurejea katika ardhi yao ya asili, na wanakusudia kung'oa utamaduni wa muqawama na mapambano miongoni mwa kizazi cha vijana cha Palestina."

Qalibaf amebainisha kuwa Bunge la Iran linaamini kuwa mapambano au muqawama ndiyo njia pekee ya kukabiliana na kujitanua kwa Wazayuni, lakini wakati huo huo linapendekeza rasmi kura ya maoni ya kitaifa Palestina ambayo ni mpango wa kisiasa na kidemokrasia na unaozingatia kanuni za sheria za kimataifa.

Wiki iliyopita, vikosi katili vya Israel vilivyojihami vikali vilivamia Msikiti wa al-Aqsa mara mbili, na kujeruhi makumi ya waumini Wapalestina na kuwakamata  mamia, waliokuwa wakisali katika eneo la tatu takatifu la Uislamu.

Picha za mashambulizi hayo zilionyesha waumini wa Kipalestina waliozuiliwa wakiwa wamelala kifudifudi huku miguu na mikono yao ikiwa imefungwa nyuma ya migongo yao, na wengine wakiwa wamefungwa mikono wakiingizwa kwenye magari ya polisi

Ghasia hizo zimetkea wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, baada ya mwaka mmoja wa umwagaji damu mkubwa uliotolekezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wa Palestina.

Utawala ghasibu wa Israel pia ulilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Syria, Lebanon na Ukanda wa Gaza baada ya makundi ya wapiganaji wa Kipalestina kurusha makombora kuelekea maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.

 

Tags