Jun 05, 2023 10:56 UTC
  • Hamas: Mauaji ya Wazayuni dhidi ya watoto wa Kipalestina yatambuliwe kuwa ni uhalifu

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetoa wito wa kutambuliwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watoto wa Kipalestina kuwa ni uhalifui na jinai, na kuwafungulia mashitaka wanaofanya jinai hizo.

Taarifa iliyotolewa na Hamas imesema kwamba, kuongezeka jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina hakutavunja azma na irada ya watu wa Palestina ya kuendeleza mapambano ya ukombozi na kupigania haki zao za kisheria, ardhi na kukomboa Msikiti wa Al-Aqsa.

Hamasi imeashiria wajibu wa kibinadamu, kisiasa na kisheria wa nchi zote, asasi za kisheria na taasisi za masuala ya kibinadamu katika uga wa kufichua jinai na uhalifu unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina, na kwa mara nyingine tena imewakumbusha walimwengu mateso, dhulma na jinai zinazoendelea kufanywa dhidi ya watoto wa Kipalestina kutokana na mashambulizi ya utawala haramu wa Israel.

Harakati hiyo imesisitiza kuwa, vitendo vya kigaidi vya utawala unaoikalia kwa mabavu Quds dhidi ya watoto wa Kipalestina vinaendelea kupitia mzingiro wa kikatili wa Ukanda wa Gaza, kwa kadiri kwamba tangu mwanzoni mwa mwaka huu, zaidi ya watoto na barobaro 28 wasio na hatia wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala huo.

Harakati ya Hamas imesisitiza kuwa, kuongezeka jinai za utawala ghasibu wa Israel kunawanyima watoto wagonjwa haki ya kupata matibabu, chakula na dawa, na kwamba vita vya utawala huo haramu dhidi ya watoto wa Kipalestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu pia vinafanyika kupitia jinai za utekaji nyara, kukamatwa, kuua kwa kufyatuliwa risasi, kufungiwa majumbani na kuwatumia watoto wa Palestina kama ngao za binadamu.

Askari wa Israel akimkaba koo mtoto wa Kipalestina

Harakati ya Hamas imesema, kimya cha jamii ya kimataifa na kutotambua uhalifu unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina kuwa ni jinai, na vilevile mienendo ya kinafiki na kindumakuwili kuhusiana na kadhia hiyo ni sawa na kuwaruhusu maafisa wa utawala huo na serikali yake ya kifashisti kufanya vitendo zaidi vya kigaidi dhidi ya watoto wasio na hatia.

Tags