Mabudha wa Myanmar waendelea kutenda jinai na mauaji dhidi ya Waislamu
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i3556-mabudha_wa_myanmar_waendelea_kutenda_jinai_na_mauaji_dhidi_ya_waislamu
Hali ya Waislamu wa Myanmar imeripoti kuwa inaendelea kutia wasiwasi licha ya ushindi wa chama cha National League for Democracy kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi ambao umekomesha utawala wa kipindi kirefu wa kijeshi nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2016 23:08 UTC
  • Mabudha wa Myanmar waendelea kutenda jinai na mauaji dhidi ya Waislamu

Hali ya Waislamu wa Myanmar imeripoti kuwa inaendelea kutia wasiwasi licha ya ushindi wa chama cha National League for Democracy kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi ambao umekomesha utawala wa kipindi kirefu wa kijeshi nchini humo.

Ripoti zinasema kuwa katika mwendelezo wa ukatili na uhalifu unaofanywa dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya, kijana mmoja Muislamu ameuawa kwa kupewa mateso ya kinyama ya Mabudha wa Harakati ya 969 katika jimbo la Rakhine. Jimbo hilo liko magharibi mwa Myanmar na limekuwa makazi ya idadi kubwa ya Waislamu tangu hata kabla ya uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza. Hata hivyo baada ya Myanmar kupata uhuru wanajeshi Mabudha wa nchi hiyo walianzisha mikakati ya kufuta utambulisho wa Kiislamu wa eneo hilo.

Katika kipindi chote cha Vita Baridi askari watawala wa Myanmar walikuwa wakiwakandamiza na kuwafukuza Waislamu katika makazi yao ya Rakhine na kufanya juhudi za kufuta utambulisho wa Kiislamu katika eneo hilo kwa kutegemea uhusiano wao mkubwa zama hizo na tawala za kikomunisti ikiwemo China, suala ambalo lilikosolewa sana. Sambamba na hayo nchi za Magharibi pia zimepuuza ukatili na unyama unaofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu wa Myanmar. Nchi hizo hizo za Magharibi hususan Marekani zimekua zikimuunga mkono na kumtetea Aung San Suu Kyi zikimnadi kama mtetezi wa haki za binadamu na mpinzani wa utawala wa kijeshi huko Myanmar.

Japokuwa San Suu Kyi ametumikia kifungo cha miaka 15 nyumbani kutokana na mapambano yake ya amani dhidi ya utawala wa kijeshi na tangu mwaka 2009 alitambuliwa na Wamagharibi kuwa ni mtetezi mashuhuri wa haki za kiraia nchini Myanmar lakini utendaji wake na chama chake unakwenda kinyume na matarajio ya Waislamu wanaodhulumiwa kwa miaka mingi nchini humo.

Hapana shaka kuwa watu wa Myanmar bila ya kujali kaumu na makabila yao watamuuliza Bi Aung San Suu Kyi kwamba, kwa nini Waislamu wa kabila la Rohingya ambao historia inathibitisha kuwa asili na fasili yao imekita mizizi nchini Myanmar hawatendewi uadili na usawa? Kwa nini haki zao hazilindwi na kutetewa? Au wao si wanadamu kama wengine? Je, nara za kutetea haki za binadamu zilizokuwa zikitolea na Bi Aung San Suu Kyi haziwahusu Waislamu wa kabila la Rohingya?

Kwa nini Bi San Suu Kyi ambaye amekuwa akipambana dhidi ya ubaguzi wa kidini na kikaumu kwa kipindi cha zaidi ya miongo minne anawapuuza Waislamu wa Myanmar hususan wale wa jimbo la Rakhine? Hii ni pamoja na kuwa Waislamu wengi wa jimbo hilo ni wakulima ambao wanachangia sehemu kubwa ya uzalisha wa chakula nchini Myanmar.

Waislamu wa Myanmar wamenyimwa haki ya kupata elimu na suhula nyingine nyingi za kijamii na kimsingi kwa kipindi kirefu cha utawala wa kijeshi wa Mabudha wenye misimamo mikali, kwa msingi huo ilitarajiwa kuwa Aung San Suu Kyi mwenye historia ya muda mrefu ya kupambana na udikteta angefanya jitihada za kuondoa dhulma na ubaguzi huo.

Chama cha Bi San Suu Kyi, National League for Democracy, kimeshinda asilimia 81 ya viti vya Bunge la Myanmar na kupata haki ya kuunda serikali ya nchi hiyo. Kwa msingi huo, kwa kutegemea historia ya Bi San Suu Kyi, wachambuzi wa mambo wanatarajia kwamba mwanasiasa huyo atajiepusha kufuata nyayo za watawala wa zamani wa kijeshi na kukomesha dhulma na ukandamizaji unaofanyika dhidi ya Waislamu nchini Myanmar.