Wamarekani wengi wanapinga nchi yao kuingilia masuala ya nchi za Kiislamu
(last modified Tue, 29 Mar 2016 14:18:19 GMT )
Mar 29, 2016 14:18 UTC
  • Wamarekani wengi wanapinga nchi yao kuingilia masuala ya nchi za Kiislamu

Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa yanaonesha kuwa Wamarekani wengi wanapinga nchi yao kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Kiislamu.

Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na shirika la Rasmussen Reports yanaonesha kuwa asilimia 58 ya Wamarekani wanapinga uingiliaji wa serikali yao katika nchi za Kiislamu kwa kisingizio cha kueneza demokrasia.

Asilimia 28 tu waliotoa maoni yao wameunga mkono uingiliaji unaofanywa na Marekani katika masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu, na asilimia 14 hawakuwa na mtazamo wowote juu ya suala hilo.

Uchunguzi huo wa maoni umefanywa katika kipindi cha kati ya tarehe 22 hadi 23 za mwezi huu wa Machi.

Kuhusiana na suala hilo, shirika la habari la Russia la Sputnik limeripoti kuwa sera za "kubadilisha utawala" katika nchi ambazo Marekani ina uadui nazo zimekuwa zikitekelezwa katika siasa za nje za Washington tangu zama za utawala wa Bill Clinton.

Ripoti ya shirika hilo imeashiria uvamizi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iraq na kueleza kuwa wataalamu wengi wa sera za nje za Washington wanaamini kwamba sera hizo ndizo zilizosababisha kujitokeza kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIL) na makundi mengine ya kigaidi.../

Tags