Mji mmoja nchini Bulgaria wapiga marufuku vazi la Burqa
Mji wa Pazardzhik nchini Bulgaria umepiga marufuku vazi la stara la burqa linalovaliwa na wanawake wa Kiislamu.
Meya wa mji huo Todor Popov amesema hakuna mwanamke yeyoye atakayeruhusiwa kuvaa vazi hilo la staha katika majengo na ofisi zote za umma, mashuleni, madukani, barabarani na hata kuendesha magari akiwa amevalia burqa au niqabu.
Amesema kuwa, yeyote ambaye atakiuka agizo hilo atapigwa faini. Watu 13 wanaotajwa kuwa viongozi wa kidini wanakabiliwa na mashtaka ya kueneza idiolojia na misimamo ya kufurutu ada sanjari na kuwashawishi watu kujiunga na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika mji huo.
Hii ni katika hali ambayo, mapema mwezi huu, chama cha Nationalist Patriotic Front ambacho kinaunga mkono serikali, kiliandaa muswada wa kupigwa marufuku vazi hilo la heshima nchini kote. Muswada huo ambao unasubiri baraka za bunge la nchi hiyo unapendekeza kuwa, mtu yeyote atakayewashawishi wengine kuvaa vazi la burqa au niqabu atahukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kutozwa faini.
Nchi za Magharibi zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na vitu vinavyoonekana kuwa na sura ya Uislamu ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku vazi la burqa. Tayari Canada, Ubelgiji na Ufaransa zimepiga marufuku vazi hilo la staha.