CAF: Pele atakumbukwa daima barani Afrika
Patrice Motsepe, Rais wa Shirikisho la Kandanda barani Afrika (CAF) amesema kuwa, nyota wa kandanda Pele, alikuwa na ''msukumo wa kipekee'' kwa bara la Afrika ambao utaishi milele kwenye mioyo ya wapenzi wa mpira wa miguu.
Motsepe amesema hayo wakati akizungumzia kifo cha Pele kilichotokea siku ya Alkhamisi akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kuugua saratani ya utumbo kwa zaidi ya mwaka mmoja. Amesema kifo chake ni pigo kubwa kwa wapenzi wa mpira. Rais wa Shirikisho la Kandanda barani Afrika (CAF) pia amepongeza dhamira ya Pele kuimarisha hali ya maisha ya watu masikini na waliotengwa. Pele ambaye jina lake halisi ni Edson Arantes do Nascimento, atazikwa Jumanne ijayo kwenye mji alikozaliwa wa Santos.
Kifo cha Pele, ambaye ni mtu pekee aliyeshinda Kombe la Dunia mara tatu kama mchezaji mwaka 1958, 1962 na mwaka 1970, kilithibitishwa kupitia akaunti yake ya mtandao wa Instagram.
Pele aliondoka kwenye umaskini hadi kuwa mmoja wa wanasoka wakubwa na wanaojulikana sana katika historia. Aliibeba Brazil hadi kwenye kilele cha soka na kuwa balozi wa kimataifa wa mchezo huo katika safari iliyoanzia mitaa ya jimbo la Sao Paulo, ambapo alicheza mpira wa kutengenezwa na soksi iliyojaa magazeti au matambara.
Pele a anabakia kuwa kinara wa ufungaji wa timu ya taifa akiwa amefunga mabao 77 katika mechi 92. Nyota wa sasa wa Brazil, Neymar, alifikisha magoli hayo kwenye Kombe la Dunia la mwaka huu nchini Qatar, akifunga bao lake la 77 katika michezo 124.
Serikali ya Rais Jair Bolsonaro, anayeondoka madarakani mnamo siku ya Jumapili, imetangaza siku tatu za maombolezo, na kusema katika taarifa kuwa Pele alikuwa mzalendo halisi, akiliinua jina la Brazil kila mahali alipokwenda.