Mufti wa Lebanon: Marekani inakwamisha zoezi la kuchaguliwa Rais wa Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i100006-mufti_wa_lebanon_marekani_inakwamisha_zoezi_la_kuchaguliwa_rais_wa_lebanon
Mufti wa Lebanon amesema kuwa, Marekani inafanya njama za kukwamisha mchakato wa kuchaguliwa Rais wa nchi hiyo na kubainisha kwamba, Washington ndio kizingiti kikuu katika uwanja huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 17, 2023 04:08 UTC
  • Mufti wa Lebanon: Marekani inakwamisha zoezi la kuchaguliwa Rais wa Lebanon

Mufti wa Lebanon amesema kuwa, Marekani inafanya njama za kukwamisha mchakato wa kuchaguliwa Rais wa nchi hiyo na kubainisha kwamba, Washington ndio kizingiti kikuu katika uwanja huo.

Sheikh Ahmad Qabalan, Mufti wa Waislamu wa Kishia nchini Lebanon ameeleza kwamba, kwa sasa nchi hiyo inakabiliwa na janga la kitaifa hususan kuhusiana na nafasi muhimu ya mamlaka ya kisiasa.

Sheikh Qabalan amesisitiza kuwa, kuna nyayo za Marekani katika masuala ya ndani ya Lebanon ambazo zinaonekana kupitia kwa baadhi ya wanasiasa ambao hawataki kuona Lebanon inafanikiwa kumchagua Rais mpya wa nchi hiyo na kuiondoa nchi hiyo katika mgogoro mkubwa.

Hivi karibuni Bunge la Lebanon lilishindwa tena kumchagua Rais mpya wa nchi hiyo kwa mara ya 12; na kupelekea mkwamo wa kumchagua kiongozi wa juu zaidi nchini humo kuendelea kushuhudiwa.

Michel Aoun, Rais wa Lebanon ambaye amemaliza muda wake

 

Muhula wa urais wa rais wa sasa wa Lebanon Michel Aoun, ulimalizika tangu tarehe 31 Oktoba mwaka jana; na kushindwa kumchagua rais mpya kunashadidisha mgogoro wa ombwe la kisiasa la nchi hiyo kubaki bila ya rais.

Bunge la Lebanon linapaswa kumchagua Rais mpya mwezi mmoja kabla ya kumalizika kipindi cha uongozi wa Rais aliyeko madarakani. Aidha kwa mujibu wa katiba, Rais wa nchi anapaswa kuchaguliwa kutoka miongoni mwa Wakristo wa Kimaroni.

Kutumbukia Lebanon katika mkwamo wa kushindwa kumchagua Rais mpya kunaifanya anga ya kisiasa ya nchi hiyo kuzidi kuwa tete sambamba na kuongeza matatizo ya kiuchumi ambayo tayari yanaiandama nchi hiyo hivi sasa.