Muhammad Shia al-Sudan: Msimamo wa Iraq kuhusu Palestina ni thabiti
Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa, msimamo wa nchi yake kuhusiana na malengo matukufu ya Palestina ni thabiti na si wenye kutetereka.
Muhammad Shia al-Sudani amesema hayo mjini Damascus Syria katika mazungumzo yake na Rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad na kusisitiza kwamba, Iraq inapinga vikali kukaliwa kwa mabavu Palestina kunakofanywa na Israel.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rais Assad wa Syria, Waziri Mkuu wa Iraq amesisitiza kwamba, wananchi wa Iraq wanajifakharisha kusimama kidete wananchi wa Syria katika kukabiliiana na mashambulio makali zaidi ya kigaidi.
Kadhalika amesema kuwa, kuna haja ya kuweko uratibu baina ya mataifa haya mawilii ya Kiarabu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbalimbali na kwamba, amani na uthabiti ni mambo mawili ambayo yanapelekea kuweko mfungamano zaidi na kwa minajili hiyo kuweza kukabiliana ipasavyo na changamoto ya ugaidi.

Kwa upande wake Rais Bashar al-Assad wa Syria ambaye serikali yake imepata ushindi baada ya kuvuka salama changamoto kubwa ameashiria historia kongwe ya uhusiano wa nchi mbili na kwamba, Baghdad ilikuwa pamoja na Damascus katika vita dhidi ya ugaidi.
Muhammad Shia al-Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq jana Jumapili aliwasili Damascus mji mkuu wa Syria ikiwa ni safari ya kwanza ya Waziri Mkuu wa Iraq nchini Syria baada ya kupita zaidi ya miaka 12.