YouTube yafunga mitandao 18 ya harakati ya Ansarullah ya Yemen
Idara ya Habari za Vita vya Yemen imetangaza kuwa kampuni ya YouTube imechukua hatua ya uhasama ya kufunga mitandao 18 inazohusishwa na Ansarullah.
Ni baada ya kampuni ya YouTube kufunga mitandao 18 ya idara hiyo na harakati ya Ansarullah ya Yemen na vilevile kitengo cha masuala ya uzalishaji na utengenezaji wa filamu za matukio ya kweli (documentary) zinazohusiana na mashahidi wa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na idara hiyo imesema, kufunga mitandao hiyo ni kitendo cha kigaidi, ambacho kwa mara nyingine kinathibitisha dhamira ya uadui ya muungano vamizi wa Saudi-Imarati dhidi ya Yemen.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, muungano wa vita wa Saudia unalenga kudhibiti vyanzo vya habari ili kuvitumia vyanzo hivyo katika kuhudumia mradi wake wa kikoloni nchini Yemen. Imeongeza kuwa, vitendo vya kampuni ya YouTube kwa mara nyingine vimeonyesha uongo wa kaulimbiu za nchi za Magharibi na washirika wao eti za kutetea uhuru wa kujieleza.
Kulingana na ripoti hiyo, idadi ya watumiaji wa mitandao iliyofungwa na YouTube inafikia zaidi ya watu laki tano 5. Mitandao hiyo inajumuisha video zaidi ya elfu saba, ambazo zimetazamwa mara milioni 90.