Askari katili wa Israel waua vijana wa Kipalestina huko Ramallah
Wanajeshi katili wa utawala haramu wa Israel wamewaua shahidi kwa kuwapiga risasi vijana wawili wa Kipalestina na kuwajeruhi vibaya wengine kadhaa wakati wa mashambulizi katika mji ulioghusubiwa wa Ukingo wa Magharibi wa Ramallah.
Shirika rasmi la habari la Wafaa la Palestina liliinukuu Wizara ya Afya ikisema siku ya Ijumaa kuwa vikosi vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimevamia kijiji cha Umm Safa, kaskazini mwa Ramallah.
Taarifa hiyo imesema jeshi la Israel liliwashambulia wakaazi kwa "risasi hai, vitoa machozi na maguruneti." Wizara ya Afya ilisema watu wawili walifikishwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya ya risasi kichwani na tumboni. Mmoja wa waliojeruhiwa, aliyetambuliwa kama Muhammad Fouad al-Bayed aliyekuwa na umri wa miaka 17 kutoka kambi ya wakimbizi ya al-Jalazoun kaskazini mwa Ramallah, alifariki dunia kutokana na majeraha yake mabaya kichwani muda mfupi baada ya kufika hospitali, kwa mujibu wa shirika la habari.
Makumi ya wengine pia walisemekana kukosa hewa kutokana na kuvuta gesi ya machozi. Umm Safa kwa muda wa wiki kadhaa zilizopita limekuwa eneo la ghasia zilizoongezeka za vikosi vya Israeli na mashambulizi ya walowezi, ikiwa ni pamoja na kuchomwa moto nyumba na magari na matumizi ya moto dhidi ya wakaazi.
Abdel Jawad Hamdan Saleh, Mpalestina aliyekuwa na umri wa miaka 24, alipigwa risasi na kufa baada ya kulengwa na moto wa Israel katika kijiji cha Ukingo wa Magharibi mapema mwezi huu. Shirika rasmi la habari la Palestina Wafa liliripoti kuwa ufyatuaji risasi huo ulifanyika Ijumaa jioni.
Aidha wanajeshi katili wa Israel wamemuua kijana mwingine wa Kipalestina wakati wa uvamizi katika mji wa Sebastia, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, saa chache tu baada ya wanajeshi wa utawala huo kumuua kijana wa Kipalestina kama sehemu ya mashambulizi yao makali katika ardhi hiyo inayokaliwa kwa mabavu.
Wizara ya Afya ya Palestina ilimtaja Mpalestina aliyefariki dunia kuwa Fawzi Hani Makhalafa mwenye umri wa miaka 18.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ilieleza masikitiko yake juu ya mauaji hayo na kusema jinai za utawala huo "haziwezi kuzima mapinduzi ya Wapalestina."
Taaarifa ya Hamas imeongeza kuwa, "Uhalifu unaoongezeka wa utawala vamizi wa Israel katika ardhi yetu yote inayokaliwa kwa mabavu hautazima mapinduzi ya watu wetu, lakini utaongeza miale yake."
Harakati ya Hamas imesema Israel lazima ijue kwamba mapambano ya Wapalestina yataendelea hadi "kutimizwa kwa matarajio ya watu wetu ya uhuru na kujitawala kwa kuanzisha Dola la Palestina na Jerusalem [al-Quds] kama mji mkuu wake."
Mauaji ya hivi punde yametokea siku moja baada ya wanajeshi wa Israel kuvamia mji wa Nablus kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kukabiliana na Wapalestina na kuua kijana mmoja na kuwajeruhi wengine wanne. WAFA iliripoti kuwa Bader Sami Masri aliyekuwa umri wa miaka 19 alipigwa risasi na askari katili wa Israel na kupelekwa hospitalini, ambapo baadaye alikufa kutokana na majeraha yake. Takriban Wapalestina 200 wameuawa na Israel tangu mwanzoni mwa mwaka huu.