Jul 22, 2023 11:09 UTC
  • Yemen yapiga marufuku bidhaa za Sweden kwa kuvunjia heshima Qurani

Serikali ya Uokovu wa Kitaifa wa Yemen imepiga marufuku bidhaa za Sweden kuigizwa nchini humo, kama jibu kwa hatua ya nchi hiyo ya Ulaya ya kuruhusu vitendo vichafu vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Shirika la habari la Iran limenukuu ripoti ya televisheni ya Al-Mayadeen inayosema kuwa, Wizara ya Viwanda na Biashara ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa wa Yemen imechapisha orodha ya kampuni za Sweden ambazo zimewekwa kwenye orodha ya vikwazo ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen imethibitisha habari hiyo na kueleza kuwa, mashirika hayo ya Sweden hayataruhusiwa kusafirisha bidhaa kwenda katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Wakati huohuo, Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetoa mwito kwa nchi za Kiislamu kukata uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia na Sweden, ili kuiadhibu nchi hiyo kwa hatua yake ya kuruhusu kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu.

Yemen imechukua hatua hiyo baada ya kafiri Salwan Momika, juzi Alkhamisi kukivunjia tena heshima Kitabu Kitakatifu cha Waislamu bilioni mbili dunia kwa ulinzi kamili wa jeshi la polisi la Sweden mjini Stockholm, kama ambavyo pia aliivunjia heshima bendera ya Iraq mbele ya ubalozi wa nchi hiyo mjini humo.

Waislamu wamejitokeza kote dunia kuitetea na kuiadhimisha Qurani Tukufu

Waislamu katika mitandano ya kijamii wameendeleza kampeni kubwa ya dunia nzima ya kutaka kususiwa bidhaa zinazozalishwa na Sweden, kulalamikia wimbi la vitendo vya kudhalilisha na kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini humo. Baadhi yao wametaka kukatwa uhusiano kati ya nchi za Kiislamu na Uswidi kulalamikia uafriti huo.

Jana Ijumaa, baadhi ya serikali za nchi za Waislamu kama Iran, Uturuki, Qatar, na Saudi Arabia zililaani na kupinga dharau na utovu wa adabu uliofanyika huko Sweden dhidi ya Quran Tukufu, ambapo baadi yazo zilikabidhi malalamiko yao rasmi kwa mabalozi wa nchi hiyo katika nchi zao.

 

Tags