Hamas: Israel ni utawala wa Kifashisti
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, Israel ni utawala wa kifashisti na kwamba harakati hiyo itaendelea kuwaunga mkono na kuwasaidia wanamapambano wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Shirika la habari la al Shahab la Palestina limenukuu Khalil al-Hayya, Naibu wa Mkuu wa Harakati ya HAMAS akisema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa, kadhia ya Palestina ndicho kitovu cha masuala ya kisiasa katika eneo hili zima na itaendelea kuwa kielelezo kikuu cha kihistoria cha zama hizi.
Amesisitiza kuwa, viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel hawapaswi kupokewa katika miji mikuu ya nchi za Waislamu na Waarabu kutokana na jinai za kupindukia wanazowafanyia Wapalestina.
Kiongozi huyo wa ngazi za juu ya Harakati ya Mapambano ya Palestina HAMAS amegusia pia jinsi wanamapambano wa Palestina wanavyozidi kupata nguvu siku baada ya siku na kusema: "Ni sawa kwamba utawala wa Kizayuni ni wa kifashisti lakini taifa la Palestina nalo lina uwezo wa kukabiliana na mafashisti hao kwa njia yoyote ile."
Amesema, tunachopigania sisi HAMAS ni kuweko mtazamo mpano wa kitaifa kati ya pande na makundi yote ya Palestina katika kupambana na utawala wa Kizayuni na serikali yake ya kifashisti inayoongozwa na Benjamin Netanyahu.
Vilevile amesema, mapenzi ya wananchi wa Palestina kwa makundi ya muqawama yanaongezeka siku baada ya siku na hayo ni mafanikio makubwa yaliyopatikana hivi sasa. Amesema, HAMAS itashiriki katika kikao cha Makatibu Wakuu wa makundi ya Palestina kinachotarajiwa kufanyika Cairo mji mkuu wa Misri.