Walowezi wa Kizayuni wavamia tena msikiti mtakatifu wa al-Aqswa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i100640-walowezi_wa_kizayuni_wavamia_tena_msikiti_mtakatifu_wa_al_aqswa
Walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada kwa mara nyingine tena wameuvamia msikiti wa al-Aqswa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kulivunjia heshima eneo hilo takatifu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 03, 2023 07:46 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni wavamia tena msikiti mtakatifu wa al-Aqswa

Walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada kwa mara nyingine tena wameuvamia msikiti wa al-Aqswa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kulivunjia heshima eneo hilo takatifu.

Idadi kubwa ya walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kuchupa mpaka asubuhi ya leo waliuvamia msikiti wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu na kufanya vitendo vya kichochezi huku wakiwa wanapatiwa ulinzi na vikosi vya usalama vya utawala haramu wa Israel.

Msikiti wa al-Aqsa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa eneo takatifu la Quds na utawala wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo, lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kupelekea njama zake kushindwa.

Ikiwa ni katika kuendeleza njama hizo leo Alkhamisi kundi moja la walowezi wa Kizayuni limeingia tena katika msikiti huo mtakatifu huku likiwa linapewa ulinzi na jeshi la utawala wa Kizayuni.

Uvamizi huo unajiri siku moja tu baada ya uvamizi mwingine kama huo Jumatano ya jana ambapo, kwa mujibu wa ripoti, Isaac Wasserlauf, mmoja wa mawaziri wa baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo, alikuwa miongoni mwa Wazayuni  walioingia na kuuvunjia heshima msikiti huo mtakatifu.

 

Vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.