Wabahrain waandamana kuunga mkono Qur'ani Tukufu
Wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano ya kulaani vikali vitendo vya mara kwa mara vya kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu nchini Uswidi na Denmark.
Waandamanaji hao waliingia barabarani katika miji mikuu ya Bahrain, Manama baada ya Sala ya Ijumaa ili kuunga mkono kitabu kitukufu cha Kiislamu na matukufu ya Kiislamu.
Wakiwa wameshikilia Qur’ani Tukufu mikononi mwao, washiriki walipiga nara za kuunga mkono Uislamu na kukemea jinai ya kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu katika nchi za Magharibi.
Waandamanaji hao pia walishikilia picha za kiongozi mkuu wa Kiislamu nchini Bahrain Sheikh Isa Qassim, ambaye alikemea uchomaji wa Qur’ani Tukufu na kuutaja kuwa ni "upuuzi mbaya wa kale."
Chini ya ulinzi wa polisi siku ya Alhamisi, wanachama wa "Danske Patrioter" - kikundi cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Denmark na kinachopinga Uislamu - waliendelea na kitendo kilicholaaniwa na wengi cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu kwa siku ya nne mfululizo katika mji mkuu wa Denmark Copenhagen.
Kundi hilo la watu wenye siasa kali walichoma kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu mbele ya balozi za Uturuki, Iraqi, Misri, Saudi Arabia na Iran huku wakitoa nara dhidi ya Uislamu.
Kundi hilo lenye msimamo mkali pia lilitangtaza moja kwa moja kitendo hicho cha kufuru kwenye akaunti yake ya Facebook.
Mapema siku hiyo, mwanamke wa Uswidi mwenye umri wa miaka 47 aliinajisi Qur'ani Tukufu huko Bromma, magharibi mwa Stockholm, chini ya ulinzi kamili wa polisi wa Uswidi.
Siku ya Jumatatu, wakimbizi wawili wanaoishi Uswidi walichoma nakala za Qur'ani Tukufu nje ya Bunge la Uswidi mjini Stockholm baada ya polisi kutoa kibali hicho. Mmoja wa watu hao ametekeleza vitendo hivyo mara mbili katika siku 40 zilizopita, nje ya msikiti mkuu wa Stockholm na baadaye nje ya ubalozi wa Iraq.
Vitendo hivyo vya kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu vimechochea hasira ya jamii nzima ya Waislamu duniani kote. Nchi kadhaa zimewaita au kuwafukuza mabalozi wa Uswidi na Denmark.
Tawala za nchi za Nordic zimedai kuchikizwa na vitendo vya kuvunjia heshima Qur’an Tukufu lakini zimedai kuwa haziwezi kuizuia chini ya sheria za kikatiba zinazolinda uhuru wa kujieleza.