Mwanamitindo Mzayuni aliyejipenyeza kama mwizi atimuliwa nchini Misri
Maafisa wa hoteli moja nchini Misri wamemfukuza mwanamitindo maarufu wa Kizayuni baada ya kugundua utambulisho wake. Mzayuni huyo aliingia Misri kwa paspoti nyingine na alificha Uzayuni wake.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, mwanamitindo huyo maarufu wa Kizayuni jana Jumapili aliliambia gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post kwamba amefukuzwa nchini Misri na kwamba maafisa wa hoteli moja mjini Cairo walimtupa nje walipomgundua tu kuwa yeye ni Mzayuni.
Mzayuni huyo amesema, alielekea nchini Misri kuhudhuria tamasha la mwanamuziki wa Kimarekani Travis Scott, lakini tamasha la mwanamuziki huyo lilikatishwa.
Amesema baada ya kusitishwa tamasha hilo aliamua kuingia mjini Cairo kuangalia mandhari mbalimbali, lakini aliporejea hotelini wasimamizi wa hapo walimtimua na kumweleza kuwa hatakiwi kukaa hata kwa sekunde moja hotelini hapo.
Maafisa wa hoteli hiyo ya Misri wamesisitiza kuwa awali hawakujua uraia wa asili wa Mzayuni huyo kwa sababu aliingia na pasi ya kusafiria inayoficha Uzayuni wake. Lakini mara baada ya kujua kuwa ni Mzayuni wamechukua hatua za haraka za kumtimua.
Mwanamitindo huyo Mzayuni ameliambia gazeti la The Jerusalem Post kuwa anajisikia vibaya sana na anaamini kuwa amedhalilishwa.
Amesema kuwa, katika kipindi cha miaka minne ya kuwa kwake maarufu, hajawahi kupata matatizo yanayotokana na Uzayuni wake, lakini mara hii mambo yamekuwa tofauti.
Amesema: (Baada ya kutimuliwa) niliondoka hotelini na kwenda moja kwa moja uwanja wa ndege."
Kufukuzwa kwa mwanamitindo huyo wa Israel kunakuja katika wakati ambapo hisia dhidi ya Wazayuni zimeongezeka kwa kiasi kikubwa katika jamii ya Misri. Wakati huo huo, mauaji ya askari watatu wa Kizayuni kwenye mpaka na Misri yaliyofanywa na askari wa mpakani wa Misri aitwaye "Mohammed Salah" tarehe 3 Juni mwaka huu, yalizua wimbi jipya la hasira za vijana wa Misri dhidi ya Wazayuni makatili ambao kila leo wanamwaga damu za Wapalestina.
Baada ya tukio hilo, tovuti ya televisheni ya Al Jazeera ya Qatar iliandika katika ripoti yake kwamba: "Wamisri wanamchukulia mwanajeshi wao aliyeuawa shahidi, Muhammad Salah kuwa ni shujaa wa taifa na ni fakhari kwa ulimwengu wa Kiarabu, ambaye aliendesha operesheni ya kijasiri dhidi ya jeshi la utawala wa Kizayuni."