Silaha za CIA na Saudia zaibwa Syria na kutumiwa kuulia Wamarekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i10102-silaha_za_cia_na_saudia_zaibwa_syria_na_kutumiwa_kuulia_wamarekani
Ripoti mpya iliyotolewa na gazeti la New York Times la nchini Marekani inaonesha kuwa, silaha ambazo zilitumwa na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA na Saudia kwa magaidi, zimeibwa na kuuzwa kimagendo nchini Jordan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 27, 2016 23:36 UTC
  • Silaha za CIA na Saudia zaibwa Syria na kutumiwa kuulia Wamarekani

Ripoti mpya iliyotolewa na gazeti la New York Times la nchini Marekani inaonesha kuwa, silaha ambazo zilitumwa na Shirika la Kijasusi la Marekani CIA na Saudia kwa magaidi, zimeibwa na kuuzwa kimagendo nchini Jordan.

Kwa mujibu wa gazeti hilo maarufu la Marekani, silaha hizo za Marekani na Saudia ambazo walitumiwa magaidi wanaofanya mauaji nchini Syria, zimeibwa na maafisa wa kijasusi wa Jordan na hivi sasa zinauzwa kimagendo nchini humo.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, baadhi ya silaha hizo zilitumika katika mauaji ya Wamarekani wawili mwezi Novemba mwaka jana na mauaji ya watu wengine watatu katika kituo kimoja cha mafunzo ya polisi cha mjini Amman, Jordan.

Mauaji hayo yalitokea baada ya afisa mmoja wa Jordan kuwashambulia maafisa usalama wawili wa serikali ya Marekani na afisa mmoja mmoja wa Afrika Kusini waliokuwa wanatoa mafunzo kwenye kituo hicho pamoja na wajordan wawili.

Marekani inagharamia kituo hicho cha mafunzo ya polisi kilichoko karibu na Amman, mji mkuu wa Jordan. Kituo hicho kilianzishwa katika viunga vya Amman, baada ya Marekani kuivamia Iraq mwaka 2003.

Ripoti ya gazeti hilo la New York Times imeongeza kuwa, serikali za Marekani na Saudi Arabia zililalamikia wizi huo, lakini malalamiko hayo hayakusaidia kitu.