HAMAS: Operesheni za silaha dhidi ya Israel hazitasimama
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa, kambi ya muqawama itaendelea kufanya operesheni zao za kimapambano kwa kutumia silaha dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Msemaji wa HAMAS, Abdul Latif al-Qanou amepongeza operesheni dhidi ya Wazayuni katika mji wa kaskazini wa Huwara, katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kueleza kuwa, operesheni hizo zinatokana na ahadi ya kundi hilo la muqawama ya kuuhami Msikiti Mtakatifu wa al-Aqsa, mkabala wa njama za Wazayuni za kuuyahudisha.
"Operesheni za silaha zitaendelea na hata kupanuliwa zaidi ili kutoa pigo kwa vikosi vya Israel na walowezi wa Kizayuni, na kuzima mpango wa serikali ya kifashisti wa eti kuunda hekalu juu ya mabaki ya Masjidul Aqsa," ameongeza al-Qanou.
Maafisa wa Israel wenye misimamo mikali na walowezi wa Kiyahudi mara kwa mara huvamia Msikiti wa al-Aqsa, kitendo cha uchochezi kinachowakasirisha Wapalestina.
Vitendo hivyo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.
Jana Jumamosi, walowezi wawili wa Kizayuni waliangamizwa kwa kupigwa risasi na mwanamapambano wa Kipalestina katika mji wa Huwara, kusini mwa Nablus na kaskazini mwa eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.