Muqawama: Hatutafumbia macho upuuzi wa kuwadhalilisha wanawake Wapalestina
Makundi ya muqawama ya Palestina yameapa kulipiza kisasi cha kudhalilishwa wanawawake wa Kipalestina katika mji wa al-Khalil, eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani kitendo cha kipumbavu kilichofanywa na wanajeshi wa Israel walipovamia jengo moja la makazi ya raia katika mji wa Al-Khalil, na kuwalazimisha wanawake watano wa Kipalestina kuvua nguo zao wakati wa upekuzi.
Harakati ya Mapmbano ya Kiislamu ya Palestina imesisitiza kuwa: Tukio hilo la kichochezi lililofanya na utawala wa kifashisti wa Israel katu halitapita hivi hivi bila kupewa jibu.
Wakati huo huo, Tarik Salami, Msemaji wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina ametoa mwito kwa Wapalestina al-Khalil na miji mingine ya Ukingo wa Magharibi kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel na kutoa jibu kwa kitendo hicho cha kudhalilishwa wanawake wa Kipalestina.
Wanajeshi wa kike wa Israel katika shambulio hilo la Julai 10, waliwalazimisha wanawake watano wa Kipalestina kuvua nguo zao na kuwatishia kwa mbwa waliopewa mafunzo walipovamia jengo la makazi ya Wapalestina katika mji wa al-Khalil.
Wanajeshi hao makatili wa Kizayuni waliwalazimisha kuvua nguo mama wa miaka 53, bintiye wa miaka 17 na mabinti wakwe zake watatu wenye miaka 20 hivi mjini al-Khalil. Juzi Jumatano pia, Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, alipozungumza na waandishi wa habari mjini New York alisema, "tukio hili lililoripotiwa linahitaji kuchunguzwa na kuhakikiwa kikamilifu."
Naye Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa UN anayehusika na masuala ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazikalowa kwa mabavu amesema ameshtushwa na tukio hilo akisisitiza kuwa, 'Hujuma dhidi ya watu na haki zao zinapasa kukoma."
Kadhalika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani kitendo hicho cha kishenzi na kutoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuishinikiza Israel iachane na tabia yake ya kukanyaga haki za binadamu kila leo huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.