Uturuki kuwasilisha OIC mpango pendekezwa wa kutatua mgogoro wa Gaza
Oct 17, 2023 12:29 UTC
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ametangaza kuwa atawasilisha katika kikao cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC mpango uliopendekezwa na nchi yake kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Gaza
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amezungumzia uungaji mkono wa Ankara kwa mpango wa kuunda serikali mbili na kupendekeza kuwa nchi za eneo hili (ikiwa ni pamoja na Uturuki) ziwe wadhamini wa upande wa Palestina na nchi zingine kadhaa ziwe wadhamini wa Israel. Kisha baada ya kufikiwa makubaliano, nchi wadhamini wa pande mbili zibebe jukumu la kutekeleza vifungu vya makubaliano yaliyofikiwa.
Huku akisisitiza umuhimu wa kuwepo mashinikizo ya kimataifa kwa Tel Aviv ili ikubali suluhisho na njia ya ufumbuzi wa kuundwa mataifa mawili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amesema, wakati umefika kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dhati ili kufanikisha kuundwa nchi ya Palestina kulingana na mipaka ya mwaka 1967, mji mkuu wake ukiwa ni Baitul Muqaddas (Jerusalem).
Fidan ameeleza kuwa, atawasilisha mpango huo uliopendekezwa wa Ankara na vipengee vyake kwa undani zaidi katika mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amebainisha kwamba utawala wa Kizayuni umevamia na kuikalia nyumba, kisha unaibomoa nyumba hiyo, na kisha unaijenga upya na kumweka mtu mwingine ndani yake ambaye unamwita mlowezi. Huo si ulowezi, huo ni wizi. Kuanzia sasa, hatua hiyo inapaswa kuitwa wizi.
Mnamo siku chache zilizopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amefanya mazungumzo kuhusu hali ya Gaza na mawaziri wenzake wa Iran, China na Russia.
Kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC kitafanyika kesho Jumatano Oktoba 18 katika makao makuu ya jumuiya hiyo Jeddah, Saudi Arabia katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama ili kuzungumzia matukio yanayojiri katika Ukanda wa Gaza.../
Tags