Ban Ki-moon: Israel iondoke katika ardhi ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i10408-ban_ki_moon_israel_iondoke_katika_ardhi_ya_palestina
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa njia pekee ya kupatikana amani ya kudumu Mashariki ya Kati ni kuundwa dola la Palestina na kurejea Israel kwenye mipaka iliyokuwepo mwaka 1967.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 02, 2016 03:31 UTC
  • Ban Ki-moon: Israel iondoke katika ardhi ya Palestina

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa njia pekee ya kupatikana amani ya kudumu Mashariki ya Kati ni kuundwa dola la Palestina na kurejea Israel kwenye mipaka iliyokuwepo mwaka 1967.

Taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambayo ilitolewa jana sambamba na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds kote duniani, imesisitiza udharura wa kufanyika jitihada kubwa za kuondoa anga mbaya inayotawala sasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.

Ban Ki-moon pia ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu ukatili na mapigano makali yanayoshuhudiwa katika siku hizi huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kulaani ukati huo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel na Wapalestina kushirikiana na Kamati ya Pande Nne inayojumuisha nchi za Marekani, Russia, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa kwa shabaha ya kukomesha mgogoro wa miaka 60 sasa wa Palestina.

Utawala haramu wa Israel umezidisha ukatili na unyama dhidi ya raia wa Palestina katika siku hizi za maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds yaliyofikia kileleni Ijumaa ya jana.

Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani ilitangazwa na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hayati Imam Ruhullah Khomeini (MA) kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds, kwa shabaha ya kuwatetea watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kupigania ukombozi wa Quds Tukufu.