Rais Erdogan wa Uturuki: Israel ni dola la kigaidi
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amesema Israel ni 'dola la kigaidi' ambalo linafanya jinai za kivita na kukanyaga sheria za kimataifa katika Ukanda wa Gaza, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Erdogan alisema hayo jana katika hotuba yake mbele ya mkutano wa wabunge wa chama tawala cha AK mjini Ankara na kueleza bayana kuwa, "Israel inafanya ugaidi wa kiserikali, nasema bayana kuwa, Israel ni dola la kigaidi."
Rais wa Uturuki amesisitiza kuwa, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS si kundi la magaidi, bali ni kundi la wapigania ukombozi.
Erdogan amesema: Wanadai kuwa HAMAS ni shirika la kigaidi, hapana, si mtandao wa kigaidi, bali ni chama cha kisiasa ambacho kinashinda uchaguzi.
Ameeleza bayana kuwa, HAMAS ni kundi la wapigania ukombozi na mujahidina wanaopambana kulinda ardhi na taifa lao. "Uturuki itaendelea kufanya juhudi kuhakikisha kuwa dunia inaitambua Israel kama dola la kigaidi," ameongeza Erdogan.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Erdogan alitoa mwito kwa mataifa ya Waislamu kushirikiana na kuwa kitu kimoja katika kukomesha jinai za kutisha zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Hii ni katika hali ambayo, licha ya viongozi wa Uturuki kujionyesha kuwa ni watetezi wa taifa madhulumu la Palestina, lakini wakati huo huo wanajaribu kupanua uhusiano na utawala huo wa kibaguzi kwa kuimarisha ushirikiano wao wa kiuchumi na kusafirisha bidhaa za kimsingi kwa utawala huo katili.