Mlipuko nje ya ubalozi mdogo wa Marekani Jeddah, Saudi Arabia
Bomu limelipuka nje ya jengo la ubalozi mdogo wa Marekani mjini Jeddah, Saudi Arabia na kuwajeruhi maafisa wawili wa polisi.
Taarifa zinasema mshambuliaji alijilipua mapema Jumatatu asubuhi nje ya jengo hilo baada ya kusimamishwa na maafisa wa polisi waliokuwa wakilinda doria katika eneo hilo. Hakuna kundi lolote lililodia kuhusika na mlipuko huo.
Imedaiwa kuwa mshambuliaji huyo alikuwa akiendesha gari kuelekea msikiti ulio karibu na ubalozi huo wakati aliposimaishwa na polisi.
Ubalozi huo umefungwa na wafanyakazi wake kupelekwa eneo lisilojulikana.
Saudi Arabia imekuwa ikikumbwa na mashambulio ambayo yamepelekea makumi ya watu kuuawa huku kundi la kigaidi la ISIS au Daesh likidai kuhusika.
Mwezi uliopita Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia ilisema kumejiri mashambulizi 26 ya kigaidi nchini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.