Afisa wa WHO: Tunashuhudia umwagaji damu wa kutisha huko Gaza
Mratibu wa timu za matibabu ya dharura katika Shirika la Afya Duniani, Sean Casey, ambaye ameshiriki katika operesheni ya kibinadamu katikati mwa Gaza, amesema damu zimetapakaa kila mahali katika hospitali za eneo hilo na kwamba alichokiona huko ni mito ya damu na chinjachija ya binadamu" akisisitiza kwamba hakuna mahali salama katika eneo hilo.
Casey amesema katika mahojiano na tovuti ya "United Nations News", baada ya ziara yake katika Hospitali ya Al-Aqsa katika mji wa Deir al-Balah katikati mwa Ukanda wa Gaza, Jumatatu iliyopita, kwamba: "Ni umwagaji damu, kama tulivyosema hapo awali. Ni mauaji na tukio baya sana."
Amesema kuwa aliyaona hayo pia katika Hospitali ya Al-Shifa iliyoko kaskazini, na pia katika hospitali mbili kubwa zaidi za kusini mwa Gaza, ambazo ni Hospitali ya Gaza European na Nasser Medical Complex.
Ameongeza kuwa "hakuna mahali salama katika Ukanda wa Gaza." Sean Casey amesema kuwa takriban huduma zote za afya zimesimama, ama kwa sababu ya kuharibiwa vifaa, au kwa sababu wafanyikazi wamelazimika kukimbia, au kwa dawa zimekwisha na kakdhalika.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa wagonjwa katika hospitali za Al-Ahly na Al-Shifa wanasubiri kufa na kusema kuwa wagonjwa wengi wanaopaswa kuwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi wanalala kwenye foleni.
Zaidi ya Wapalestina elfu 20 wameuawa, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, katika mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.