Donald Trump asifu jinai za dikteta Saddam Hussein
Mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump amesifia jinai zilizofanywa na dikteta wa zamani wa zamani wa Iraq Saddam Hussein na kudai kuwa, kiongozi huyo aliweza kukabiliana vyema na magaidi.
Trump ambaye daima amekuwa akikosoa vikali sera za kigeni za Rais Barack Obama na Hillary Clinton wakati akiwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ametoa matamshi hayo ya ajabu katika hotuba yake Bw kwenye mkutano wa kampeni eneo jimbo la North Carolina na kusifu jinai za dikteta huyo wa zamani wa Iraq aliyeuawa kwa kunyongwa Desemba 2006.
Trump amenukuliwa akisema: "“Saddam Hussein alikuwa mbaya, sio ndio? … Lakini mnafahamu ni jambo gani aliweza kulifanya vyema sana? Aliwaua magaidi tena alifanya hivyo kwa ufanisi kabisa. Hakuna mtu aliyewakumbusha kuhusiana na haki zao, na wao hawakusema kitu, walikuwa magaidi, na kila kitu kikaisha."
Trump ambaye amekuwa akitoa matamshi ya ajabu ajabu amewahi kusema kwamba ulimwengu ungelikuwa bora kwa asilimia 100 kuliko sasa lau madikteta kama Saddam Hussein na kanali Muammar Gaddafi wangelikuwa bado wako uongozini.
Akijibu matamshi hayo ya Donald Trump, mshauri wa zamani wa kisiasa wa Hillary Clinton amesema kuwa, matamshi hayo yanaonyesha ni jinsi gani itakuwa hatari kamaTrump atakuwa Amiri Jeshi Mkuu na inadhihirisha kwamba, hana sifa ya kuhudumu kama rais.