Sana'a: Marekani ni tishio la kwanza kwa meli katika Bahari Nyekundu
Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imepongea msimamo wa Saudi Arabia kuhusu Bahari Nyekundu na kusema, Marekani ndio tishio la kwanza na pekee la usalama wa safari za meli.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imetangaza kuwa:,"Usafirishaji katika Bahari Nyekundu ni muhimu na tumesisitiza mara kwa mara kwamba usafirishaji katika eneo hili ni salama kabisa."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen imeongeza kuwa, kwa vyovyote vile, Yemen haiwezi kukaa kimya mbele ya mashambulizi yanayofanywa dhidi yake, na hili halitaathiri msimamo wa Sana'a wa kuitetea Gaza na Palestina.
Kuhusiana na suala hilo, Hussein al Azzi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Yemen amepongeza msimamo wa kishujaa wa Saudi Arabia kuhusu kadhia ya Bahari Nyekundu.
Saudi Arabia imekataa kushiriki katika muungano wa Marekani na Uingereza wa kuiunga mkono Israel na kuishambulia Yemen. Muungano huo uliundwa kwa ushirikiano wa nchi kadhaa za Magharibi na Bahrain. Hadi sasa muungano huo umetekeleza mashambulizi mengi dhidi ya Yemen.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesisitiza ulazima wa kuziunga mkono harakati za upinzani huko Marekani na Uingereza katika juhudi za kupinga hatua za kiuhasama na uvamizi za nchi mbili hizo katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Katika upande mwingine, Muhammad al Bukhaiti mwakilishi wa ngazi ya juu wa harakati ya Ansarullah ya Yemen ameashiria taarifa iliyotolewa na Marekani na Uingereza kwamba mashambulizi ya karibuni dhidi ya Yemen yalitekelezwa na nchi hizo mbili pekee akisema kuwa hii ni ishara ya kushindwa kwa muungano huo wa Magharibi.
Vyanzo vya habari vilitangaza jana Jumatatu kwamba ndege za kivita za Marekani na Uingereza kwa mara nyingine zimeshambulia maeneo tofauti ya Yemen.
Hata hivyo vikosi vya ulinzi vya Yemen vimesema havitasimamisha mashambulizi yake dhidi ya meli za utawala haramu wa Israel katika maji ya Bahari Nyekundu hadi pale utawala huo haramu utakapokomesha mashambulio yake ya kinyama ya angani na nchi kavu dhidi ya Gaza, ambayo tangu Oktoba 7 hadi sasa yameshateketeza roho za Wapalestina wanaokaribia 30,000.