Uhispania, Ireland na Norway zaitambua rasmi Palestina
(last modified Wed, 29 May 2024 03:47:26 GMT )
May 29, 2024 03:47 UTC
  • Uhispania, Ireland na Norway zaitambua rasmi Palestina

Uhispania, Ireland na Norway jana zilipasisha rasmi mpango wa kutambua rasmi Palestina, katika uamuzi ulioratibiwa hatua ambayo imeongeza himaya na uungaji mkono kwa Palestina barani Ulaya.

Baada ya serikali ya Ireland kuidhinisha rasmi hatua hiyo, Waziri Mkuu Simon Harris amesema lengo ni kuweka hai matumaini ya amani ya Mashariki ya Kati.

Harris alisema walitaka kuitambua Palestina mwishoni mwa mchakato wa amani, lakini wamechukua hatua hiyo pamoja na Uhispania na Norway ili kuweka hai muujiza wa amani, huku akiutolea  wito utawala ghasibu wa Israel kukomesha janga la kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Baada ya hatua ya Norway kuitambua rasmi Palestina kuanza kutekelezwa, Waziri wa Mambo ya Nje Espen Barth Eide alipongeza hatua hiyo na kuitaja Jumanne ya jana kuwa siku maalumu kwa uhusiano wa Norway na Palestina.

Wakati huo huo, baada ya baraza la mawaziri la Uhispania kuunga mkono mpango wa nchi hiyo wa kuitambua rasmi Palestina, Waziri wa Mambo ya Nje Jose Manuel Albares alisema ni siku ambayo itaangaziwa katika historia ya Uhispania.

Bendera ya Palestina

 

Hapo awali, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alisema kutambuliwa rasmi taifa la Palestina ni muhimu kwa amani, akisisitiza kwamba hatua hiyo haijachukuliwa dhidi ya Israel na kwamba ndiyo njia pekee ya kuhakikisha mustakabali wa mataifa mawili yanayoishi bega kwa bega kwa amani na usalama.

Wimbi la mataifa mbalimbali kuitambua Palestina hususan barani Ulaya limeshika kasi hivi sasa na kuutia kiwewe utawala ghasibu wa Israel hasa kutokana na kuongezeka himaya na uungaji mkono wa walimwengu kwa taifa madhuluumu la Palestina.