Taathira za kiuchumi za mashambulio ya mrengo wa Muqawama katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu
(last modified Tue, 16 Jul 2024 06:34:13 GMT )
Jul 16, 2024 06:34 UTC
  • Taathira za kiuchumi za mashambulio ya mrengo wa Muqawama katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu

Bandari ya Eilat iliyoko katika mji wa kusini zaidi mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, imefungwa na kutangaza kufilisika kutokana na mashambulizi ya muqawama wa Yemen na Iraq.

Bandari ya Eilat ilitangaza kufilisika kutokana na kupungua kwa shughuli za kibiashara na mapato baada ya kuongezeka mashambulizi ya muqawama wa Yemen na Iraq. Huku meli zinazoelekea katika bandari za utawala wa Kizayuni zikendelea kulengwa na mhimili wa muqawama wa Yemen na Iraq katika Bahari Nyekundu, meli nyingi za kibiashara zimebadili mkondo na kulazimika kupitia njia ya mbali zaidi ili kutia nanga katika Bahari ya Mediterania, jambo ambalo linaongeza maradufu gharama na muda wa kufikisha bidhaa kwa wafanyabiashara wa Kizayuni. Gideon Gulbert, Mkurugenzi Mtendaji wa Bandari ya Eilat, alitangaza katika kikao cha Kamati ya Masuala ya Kiuchumi ya Knesset kilichofanyika Julai 7 kwamba Bandari ya Eilat haijapata shughuli yoyote au mapato kwa muda wa miezi minane iliyopita.

Mashambulio ya vikosi vya Ansarullah ya Yemen dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari Nyekundu yamepelekea kupungua kwa asilimia 85 ya kiwango cha biashara kupitia bandari za utawala ghasibu wa Israel, na hivyo kupungua kwa kiasi kikubwa biashara inayofanyika katika bandari hizo, jambo ambalo limeilazimisha bandari ya Eilat kuomba msaada wa kifedha kutoka baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni. Huku likiendelea kusisitiza marufuku ya meli za utawala wa Kizayuni au meli zinazoelekea katika bandari za Palestina inayokaliwa kwa mabavu kupitia baharii hiyo hadi pale utawala huo utakaposimamisha mzingiro na mauaji ya umati dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza, jeshi la Yemen limetangaza kuwa meli nyingine zote ziko huru kupita katika maji ya bahari hiyo.

Bandari ya Eilat katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu

Kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba (2023), makundi ya muqawama ya eneo yamechukua hatua ya kuunga mkono makundi ya muqawama ya Palestina na hivyo kutoa pigo kubwa lisilofidika dhidi ya utawala wa Kizayuni. Hali ya kiuchumi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu ni mbaya sana, na kuendelea vita vya Gaza, kumepelekea pia baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu lichukiwe na kupoteza uungaji mkono kati ya Wazayuni.

Yali Rotenberg, Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya utawala wa Kizayuni amekiri kuwa nakisi ya kifedha ya utawala huo imefikia takriban dola bilioni 30. Kabla ya mashambulizi ya jeshi la Kizayuni huko Gaza, uchumi wa utawala huo ulikuwa unakabiliwa na mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa, ughali wa maisha, mishahara duni na kupungua kwa viwango vya maisha. Kwa kuendelea vita vya Gaza, masoko ya kiuchumi na kibiashara katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yamekabiliwa na mdororo mkubwa wa kiuchumi na hivyo kuwasababishia Wazayuni hasara kubwa. Vituo muhimu vya kibiadhara na kifedha vimefungwa, wafanyakazi wameacha kufanya kazi na wakandarasi pamoja na wahandisi wa miradi muhimu ya maendeleo wamesimamisha shughuli zao.

Moja ya taathira kuu za migogoro na vita vya sasa kati ya Tel Aviv na Hamas katika uchumi wa utawala wa Kizayuni ni kukimbia kwa kiasi kikubwa mitaji ya ndani na nje ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Mbali na kukimbia wawekezaji wa kigeni, wawekezaji wa ndani pia wana wasiwasi mkubwa kuhusiana na hali ya baadaye ya utawala wa Kizayuni, hivyo wamekuwa wakionyesha dalili za kukimbia kutoka ardhi hizo. Kwa mujibu wa takwimu mbalimbali hususan za mashirika ya wahajiri ya Ulaya katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, hivi sasa kasi ya uhajiri wa raia wa Kizayuni wanaokimbia ardhi zinazokaliwa kwa mabavu imeongezeka maradufu ikilinganishwa na ya kabla ya operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa.

Jeshi la Yemen likishambulia meli ya Magharibi iliyokuwa ikijaribu kuelekea katika bandari za Israel

Matokeo ya uchochezi wa vita wa baraza la mawaziri la Netanyahu na Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada ni kuporomoka kwa uchumi wa utawala wa Kizayuni katika miezi ya hivi karibuni. Kwa kuendelea vita, hata misaada ya kifedha ya Marekani na washirika wake wa Magharibi haijaweza kubadilisha hali mbaya ya kiuchumi inayoukabili utawala wa kibaguzi wa Israel. Kundi la viongozi wa Kizayuni limetahadharisha kuhusu athari mbaya za kuendelea vita huko Ghaza na uwezekano wa kusambaratika kisiasa na kiuchumi utawala wa Kizayuni.

Vita vya Gaza vimefichua mzozo wa kisiasa na kiuchumi wa Tel Aviv na bila shaka kuendelea operesheni za makundi ya muqawama katika eneo kutazidisha tu mzozo wa kiuchumi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Mivutano ya ndani katika baraza la mawaziri na tofauti za mitazamo kati ya Netanyahu na Wazayuni wenye misimamo ya kupindukia mipaka zimeibua vurugu kubwa ndani ya utawala huo, hivyo utatuzi wa changamoto za kiuchumi hautabadilisha chochote kwa manufaa ya utawala huo.